Juma Ramadhani, mjasiriamali kutoka Mkwajuni, alipongeza elimu aliyopata kuhusu Nishati Safi ya Kupikia na kuahidi kubadilisha mtindo wake wa maisha kwa kuanza kutumia nishati hiyo.
“Nimejifunza mambo mengi kuhusu faida za matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia. Nitabadilika na nitakuwa balozi wa kuhamasisha wajasiriamali wenzangu na jamii kwa ujumla juu ya matumizi ya nishati hii,” alisema Ramadhani.
Wito wa kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia umetolewa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika Kongamano la Wajasiriamali Wilaya ya Songwe, lililofanyika Agosti 16, 2025 katika kijiji cha Mkwajuni, mkoani Songwe. Kongamano hilo liliandaliwa na Mtandao wa Kuinua Wanawake Kiuchumi Tanzania (TAWEN) na kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 350.
Mtaalam wa Nishati na Jinsia kutoka REA, Dkt. Joseph Sambali, alisema kuwa wajasiriamali wana nafasi kubwa ya kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo katika mnyororo wa thamani wa sekta ndogo ya Nishati Safi ya Kupikia.
“Wajasiriamali wanayo nafasi kubwa ya kufaidika na fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani katika sekta ndogo ya Nishati Safi ya Kupikia,” alisema Dkt. Sambali.
Alitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni pamoja na uwakala na uzalishaji wa bidhaa za nishati safi ya kupikia kama vile mkaa mbadala na majiko banifu. Alisisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ni muhimu kwa ajili ya kulinda afya ya mtumiaji na mazingira.
“Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ni muhimu katika kuepusha magonjwa yanayotokana na uvutaji wa hewa chafu inayosababishwa na matumizi ya nishati isiyo salama. Pia husaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na ukataji ovyo wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa,” aliongeza Dkt. Sambali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAWEN Nyanda za Juu Kusini, Oliva Hasukenye, alisema kuwa wao kama mtandao wanaunga mkono kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia na wamejipanga kuendelea kuhamasisha jamii kupitia majukwaa mbalimbali.
“Sisi TAWEN tunaunga mkono kampeni hii ya Nishati Safi ya Kupikia kwani maisha ya kutumia nishati isiyo safi na salama tumeyaishi, madhara yake tunayajua, na tumedhamiria kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali kuelimisha jamii kuhusu madhara hayo,” alisema Hasukenye.
Aliongeza kuwa mjasiriamali anayepika kwa kutumia nishati safi hawezi kulinganishwa na yule anayetumia nishati isiyo salama, kuanzia kipato hadi usafi wa mazingira anayofanyia kazi.
Katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaendelea kutumia mbinu mbalimbali za kuelimisha, kuwezesha na kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, ili kulinda afya ya wananchi na kuhifadhi mazingira kwa ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.




0 Comments:
Post a Comment