Saturday, August 2, 2025

TUME YAUCHANGAMKIA USHIRIKIANO NA VYOMBO VYA HABARI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025



Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imevitaka vyombo vya habari nchini kuhakikisha vinatoa taarifa sahihi, kwa wakati na zenye kujenga kuhusu mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ili kuwawezesha wananchi kushiriki kwa uelewa na amani.



Akizungumza tarehe 1 Agosti 2025 jijini Dar es Salaam, katika ufunguzi wa mkutano kati ya Tume na Wahariri wa vyombo vya habari, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele alisema vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kufanikisha mchakato wa uchaguzi nchini.



"Vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya mpiga kura na taarifa sahihi zinazowawezesha kufanya maamuzi ya msingi kwa uhuru na kwa amani," alisema Jaji Mwambegele.



Aliwahimiza wahariri kutumia majukwaa yao kuwahamasisha wananchi waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kushiriki kikamilifu kwa kujitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu, utakaofanyika tarehe 29 Oktoba 2025.



Amesisitiza pia kuwa vyombo vya habari ni mshirika muhimu wa Tume, akisema:
"Ushirikiano kati ya Tume na vyombo vya habari ni nguzo muhimu katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na kwa kuzingatia sheria za uchaguzi."


Katika mada aliyoitoa kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Ramadhani, alisema vyombo vya habari ni msingi wa mafanikio ya uchaguzi wowote unaofanyika kwa uwazi na ushirikishwaji wa wananchi.



"Katika nchi yoyote inayodhamiria kufanikisha jambo kubwa kama uchaguzi, vyombo vya habari ndiyo msingi wa kwanza, kwani kupitia kwao, wananchi hupata taarifa sahihi, zilizofanyiwa utafiti na kuhakikiwa," alisema Kailima.



Aliongeza kuwa bila ushirikiano na vyombo vya habari, juhudi za Tume katika utoaji wa elimu na taarifa haziwezi kufika kwa wananchi.
"Maana yake kila kinachotolewa na Tume hakiwezi kuwafikia wananchi iwapo vyombo vya habari havitaamua jambo hilo lifanikiwe," alisisitiza.

Pia alibainisha kuwa vyombo vya habari vina wajibu wa kuibua upotoshaji wa aina yoyote unaoweza kufanywa kwa bahati mbaya au makusudi kuhusu shughuli za Tume na mchakato wa uchaguzi.

"Vyombo vya habari ndivyo vinavyoweza kuwa sauti ya kwanza ya kuonesha upotoshwaji wa aina yoyote unaofanywa kwa bahati mbaya au kwa makusudi kuhusu Tume na kuhusu zoezi la Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025," alisema Kailima.

Aliwataka wahariri kuhakikisha kuwa taarifa kuhusu uchaguzi zinatolewa mara kwa mara, ili kuwezesha wananchi kufuatilia hatua mbalimbali za maandalizi na utekelezaji wa uchaguzi huo.


"Tunawaomba na kuwanasihi, kutumia nafasi na fursa mlizonazo kuhakikisha kunakuwepo na taarifa za mara kwa mara za kuelezea kinachoendelea kuhusu uchaguzi," alisema.

Katika kikao hicho, wahariri walikumbushwa kutumia kauli mbiu ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 inayosema: “Kura Yako Haki Yako, Jitokeze Kupiga Kura” katika taarifa na vipindi wanavyoviandaa kwa lengo la kuhamasisha ushiriki wa wananchi.


No comments:

Post a Comment