Monday, August 4, 2025

Pindi Chana Ahamasisha Umma Kutembelea Maonesho ya Nanenane Kujifunza Kuhusu Uhifadhi na Utalii



Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, ametoa wito kwa Watanzania kutoka kada mbalimbali kutembelea maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane) yanayoendelea kitaifa katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, pamoja na kwenye kanda nyingine nchini, ili kujifunza kuhusu vivutio vya utalii, shughuli za uhifadhi na fursa za uwekezaji katika sekta ya maliasili na utalii.



Akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika viwanja hivyo, Chana alisema maonesho ya mwaka huu yamekuwa ya kipekee kwa kuwa yameunganisha sekta mbalimbali zinazochangia maendeleo ya nchi kupitia ushiriki wa taasisi za serikali, sekta binafsi na jamii kwa ujumla.


“Natoa wito kwa Watanzania kutembelea maonesho ya Nanenane katika kanda zote yanapofanyika ili wapate elimu ya vivutio vya utalii tulivyonavyo, fursa za uwekezaji, elimu ya uhifadhi, na ufugaji nyuki. Wizara inaendelea kuongeza mazao mbalimbali ya utalii ikiwemo utalii wa vyakula na utalii wa kilimo kwa kuwa maonesho haya yamefunganisha sekta mbalimbali ili tuendelee kutangaza nchi yetu na kupata maendeleo kwa pamoja,” alisema Dkt. Chana.



Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na taasisi zake imekuwa ikishiriki kikamilifu kwenye maonesho hayo kwa lengo la kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa rasilimali za taifa, matumizi endelevu ya maeneo yaliyohifadhiwa, pamoja na kutangaza vivutio adimu vya utalii vilivyopo nchini.


Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki maonesho hayo, ikitangaza vivutio mbalimbali vya kipekee vinavyopatikana ndani ya eneo hilo. Vivutio hivyo ni pamoja na Kreta ya Ngorongoro, Empakai, Olmoti, Mlima Lolmalasin (wa tatu kwa urefu nchini), Maporomoko ya Maji ya Endoro, na Mapango ya Tembo.


Aidha, mamlaka hiyo inatangaza vivutio vya utalii wa malikale kama Makumbusho ya Olduvai, Nyayo za Laetoli, mchanga unaohama, pamoja na utalii wa anga kupitia Kimondo cha Mbozi na Mapango ya Amboni mkoani Tanga. Mapango haya yana historia ya kipekee ikiwa ni pamoja na mchango wake katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika, na kuonesha urithi wa kihistoria wa watu wa mkoa wa Tanga.


Wageni wanaotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii pia wanapata fursa ya kuona mubashara baadhi ya vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro kupitia skrini kubwa ya televisheni iliyofungwa katika banda hilo.


Kaulimbiu ya maonesho ya Nanenane kwa mwaka 2025 ni: *“Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”*, ikiwa ni mwendelezo wa kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za uzalishaji pamoja na uongozi bora kwa maendeleo ya taifa.


No comments:

Post a Comment