Na Hamis Dambaya
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imeonyesha uzalendo na mshikamano na timu ya taifa kwa kulipia tiketi 500 za kuingilia kwa mashabiki wa soka kushuhudia pambano la robo fainali kati ya Taifa Stars ya Tanzania na Morocco, litakalofanyika usiku wa leo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Tiketi hizo zimekabidhiwa rasmi leo kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA na Meneja wa Idara ya Huduma za Utalii na Masoko, Mariam Kobelo, ambaye amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono maendeleo ya michezo nchini sambamba na kukuza utalii wa ndani.
“Tumeona ni muhimu kuhamasisha Watanzania kushiriki kwa wingi katika michezo na pia kuwatia moyo wachezaji wetu. Lakini zaidi, tunalenga kutumia jukwaa hili kutangaza vivutio vyetu vya utalii kama vile Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema Kobelo.
Kwa upande wake, "Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT)", Neema Msita, ameipongeza NCAA kwa mchango wake muhimu, akisema kuwa michuano ya **CHAN 2025** imekuwa jukwaa kubwa la kutangaza vivutio vya Afrika, na Tanzania inapaswa kutumia fursa hii kujitangaza zaidi kimataifa.
“Mashindano haya yamevuta hisia na mashabiki wengi kutoka barani Afrika na duniani kote. Ni wakati wetu kuonyesha uzuri wa nchi yetu kupitia michezo na utalii,”aliongeza Msita.
Mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Morocco ni sehemu ya hatua ya "robo fainali ya michuano ya CHAN 2025", ukiwa ni mmoja wa mechi zinazovuta hisia kubwa kutokana na umuhimu wake kwa timu ya taifa. Mechi hiyo itapigwa leo saa 2:00 usiku katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mashabiki waliolipiwa tiketi wanatarajiwa kuupa uwanja joto na hamasa kubwa huku wakiwa nyuma ya Taifa Stars katika harakati za kutinga nusu fainali ya mashindano hayo.


0 Comments:
Post a Comment