Friday, August 15, 2025

Kiwanda Kipya cha Chumvi Lishe Kigoma Kuimarisha Sekta ya Mifugo na Kupunguza Uagizaji Kutoka Nje


 Sekta ya madini nchini inaendelea kupiga hatua kubwa baada ya Kampuni ya Nyanza Salt kuzindua rasmi kiwanda cha kuzalisha chumvi lishe (Cattle Lick) kwa ajili ya mifugo, kiwanda ambacho kinatarajiwa kuongeza thamani ya chumvi inayozalishwa hapa nchini na kupunguza uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje.


Kiwanda hicho kilichopo wilayani Uvinza mkoani Kigoma, kimezinduliwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ambaye amesisitiza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha madini yote yanayopatikana nchini yanaongezewa thamani kabla ya kuuzwa au kutumika.

"Ni hatua kubwa sana kwa nchi yetu kuona bidhaa kama chumvi lishe, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiagizwa kutoka nje ya nchi, sasa inazalishwa hapa nchini. Hii si tu inaongeza thamani ya madini yetu, bali pia ni suluhisho kwa changamoto kubwa inayowakabili wafugaji wetu ambao walilazimika kununua bidhaa hiyo kwa bei ya juu kutoka nje ya nchi," alisema Mavunde.



Aidha, aliongeza kuwa serikali imejipanga kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya madini ili kuongeza uzalishaji wa chumvi ghafi na kuhakikisha viwanda vya ndani vinapata malighafi ya kutosha, na hatimaye Tanzania iweze kujitegemea kikamilifu katika bidhaa za chumvi za viwandani na lishe ya mifugo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Nyanza Salt Mines, Mukesh Mamlani, alisema uzalishaji wa chumvi lishe kutoka kwenye madini ya chumvi ya asili ni hatua ya kimkakati inayolenga kuinua ustawi wa sekta ya mifugo nchini.



"Chumvi lishe ni hitaji muhimu kwa afya ya mifugo. Kupitia kiwanda hiki, tutahakikisha tunazalisha bidhaa bora kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, ili wafugaji wa Tanzania waweze kupata bidhaa salama, bora na kwa bei nafuu. Lengo letu ni kufikia uzalishaji wa tani 120,000 za chumvi ifikapo mwaka 2027," alisema Mamlani.

Alisisitiza kuwa mradi huo si tu una faida kwa sekta ya mifugo, bali pia unachangia ukuaji wa uchumi wa eneo hilo kupitia ajira na mchango katika pato la taifa.



Naye Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Dina Mathamani, alieleza kuwa uwepo wa kiwanda hicho katika wilaya hiyo umeleta mafanikio makubwa kwa jamii ya Uvinza, hususan katika eneo la ajira na biashara ndogo ndogo.

"Kampuni ya Nyanza Salt imekuwa kichocheo cha maendeleo kwa wananchi wetu. Wakati wa msimu wa uchakataji, zaidi ya wananchi 1,000 hupata ajira ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja. Hii imeongeza kipato cha familia nyingi na kuinua hali ya maisha ya watu wetu," alisema Mathamani.

Uanzishaji wa kiwanda hiki unaonekana kuwa hatua muhimu ya kuimarisha uchumi wa ndani, kukuza sekta ya mifugo, na kuifanya Tanzania kuwa na uhuru wa kiuchumi katika bidhaa za chumvi, huku ikionyesha mafanikio ya ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi katika kuongeza thamani ya rasilimali za taifa.

No comments:

Post a Comment