KAMISHNA BADRU AWATAKA ASKARI WA UHIFADHI KUZINGATIA WELEDI KAZINI

 


Na Mwandishi Wetu – Pololeti, Ngorongoro

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Abdul-razaq Badru, ametoa wito kwa askari wa uhifadhi wanaofanya kazi katika Pori la Akiba la Pololeti Wilayani Ngorongoro kuhakikisha wanazingatia maadili, weledi na matokeo ya kazi zao ili kulinda hadhi ya jeshi hilo na kuhakikisha uhifadhi endelevu wa maliasili.



Akizungumza na askari hao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua hali ya ulinzi na uhifadhi katika eneo hilo, Kamishna Badru alisema:
"Ni muhimu kila askari kutambua nafasi yake na kutekeleza majukumu kwa uadilifu, uaminifu na kujituma. Kila mmoja wenu ni kiungo muhimu katika mafanikio ya uhifadhi nchini."


Kamishna Badru alieleza kuridhishwa na juhudi kubwa zinazofanywa na askari hao, hatua ambayo imepelekea kuongezeka kwa idadi ya wanyamapori katika eneo hilo.

"Kazi yenu inaonekana. Leo hii, Pololeti ni miongoni mwa maeneo yenye wanyama wengi na tofauti wakiwemo tembo, twiga, simba, nyumbu, swala, pofu na pundamilia. Hii ni dalili kuwa ulinzi unaimarika na mazingira ya wanyama yanazidi kuimarika," alisema.



Aidha, Kamishna Badru aliwahakikishia askari kuwa NCAA itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa kujenga miundombinu bora na kuhakikisha vitendea kazi vinapatikana ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

"Tutahakikisha kuwa mnakuwa na mazingira bora ya kufanyia kazi. Hii ni pamoja na kuboresha makazi, ofisi na vifaa vya kazi, kwa sababu askari mwenye mazingira bora atatekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi," aliongeza.



Ziara ya Kamishna Badru inalenga kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi katika maeneo yote ya NCAA, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha utunzaji wa bioanuai unaimarika huku maslahi ya askari na jamii yanazingatiwa.

0 Comments:

Post a Comment