Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Abdul-razaq Badru, ametembelea kijiji cha Msomera kilichopo wilayani Handeni, mkoani Tanga, kwa ajili ya kujionea maendeleo ya uendelezaji wa eneo hilo linalotumika kuwahifadhi wananchi wanaohamia kwa hiari kutoka Tarafa ya Ngorongoro.
Katika ziara hiyo, Kamishna Badru aliambatana na mkuu wa wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, ambapo alieleza kuridhishwa na kazi kubwa iliyofanywa na serikali katika maandalizi ya miundombinu kwa ajili ya wakazi wapya wa kijiji hicho.
"Serikali imefanya kazi kubwa. Tutaendelea kushirikiana katika kuhakikisha kijiji hiki kinakuwa bora ili wananchi waliohamia na wale watakaohamia waweze kuishi hapa kwa furaha," alisema Kamishna Badru.
Alisisitiza kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro itashirikiana kikamilifu na wizara za kisekta ili kuhakikisha Msomera inakuwa kijiji cha mfano nchini kwa kuwekewa huduma zote muhimu za kijamii.
Kwa upande wake, mkuu wa wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, alisema kuwa kazi za uboreshaji wa miundombinu zinaendelea kwa kasi, ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa nyumba na kuhakikisha zinalindwa ipasavyo.
"Kazi mbalimbali za uboreshaji wa miundombinu zinaendelea, na ulinzi wa nyumba zilizokamilika tayari umeimarishwa," alisema Nyamwese.
Kijiji cha Msomera kimekuwa mfano wa mafanikio ya utekelezaji wa sera ya serikali ya awamu ya sita, inayolenga kuweka mazingira rafiki kwa wananchi waliokubali kuhamia kwa hiari kutoka Hifadhi ya Ngorongoro, ili kupisha shughuli za uhifadhi wa mazingira na maliasili.
Kupitia juhudi hizi, serikali inalenga kuhakikisha uhifadhi endelevu wa Hifadhi ya Ngorongoro huku ikiendelea kuboresha maisha ya wananchi wanaohamia Msomera kwa kuwapatia huduma bora za kijamii kama vile maji, umeme, afya, elimu na miundombinu ya barabara.




0 Comments:
Post a Comment