📌JAMII YA KIMASAI YATOA ADHABU YA KIMILA KWA VIJANA WALIOKASHIFU RAIS SAMIA 📌Viboko Hadharani kwa Waliokiuka Maadili, 📍Onyo Kali kwa Wavamizi wa Eneo la Mila la Elerai

 


MAELFU ya vijana na viongozi wa kimila kutoka jamii ya kifugaji ya Kimasai wamekusanyika katika eneo la kimila la Elerai, jijini Arusha, kushuhudia utoaji wa adhabu ya kimila kwa vijana wawili waliotuhumiwa kutumia lugha ya matusi dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.





Vijana hao, Laurence Kuesoy na David Zakayo, wote wakazi wa Arusha, walikiri hadharani kufanya kosa hilo na kuomba msamaha mbele ya wazee wa mila, viongozi wa jamii na mamia ya wananchi waliokusanyika. 



Kila mmoja alitozwa faini ya dume moja la ng’ombe, waliyoichinja na kula kwa pamoja kama ishara ya kutubu na kurudisha heshima ya jamii.



Laigwanani Mkuu wa jamii hiyo, Isack Ole Kissongo, alisema tukio hilo lililotokea tarehe 20 Juni 2025, lilikuwa la aibu na la kuvunja maadili ya jamii ya Kimasai, ambayo imejengwa juu ya misingi ya heshima, nidhamu, na utii kwa viongozi wa taifa.


“Wiki hii tumeona kwenye video vijana wamefanya makosa makubwa ya kujirekodi na kumtusi Rais. Katika maisha yangu ya zaidi ya miaka sabini sijawahi kuona maneno hayo, hata kama tuna uhuru kiasi gani,” alisema Kissongo.


“Niliwasiliana na viongozi wa vijana na kuwaomba polisi wasiwakamate ili tukayamalize kimila. Walikubali, na tukawaandalia adhabu inayostahili kwa mujibu wa mila zetu.”

Mbali na adhabu ya faini ya ng’ombe, Laigwanani huyo alitangaza hatua kali zaidi kwa vijana wa jamii hiyo wanaoendeleza mienendo isiyofaa, ikiwemo uvutaji wa bangi, uvaaji wa suruali za mlegezo, kusuka rasta zisizokubalika na wanawake wanaovaa mavazi ya kihuni.


“Kuanzia leo, kijana atakayeonekana amesuka rasta za kisasa, aletwe hapa apigwe fimbo sabini. Ninachotaka wasuke ni rasta za Kimasai. Msichana anayepasua nguo hadi sehemu za siri, ashughulikiwe na kina mama,” alionya.


Jamii hiyo pia ilitoa msimamo wake mkali dhidi ya wavamizi wa eneo la mila la Elerai, ambalo lina zaidi ya ekari 100 na kutumika kwa shughuli za kijadi na urithi wa kitamaduni.


“Eneo hili la Elerai ni eneo la kupata mafunzo ya maadili kwa vijana. Tulivunja uzio uliozungushiwa na watu waliotaka kuuza eneo letu. Hatukubali, Wamasai hatupimwi wala hatubabaishwi. Kama mtu ana pesa, ajaribu. Hapa haingii mtu mwingine zaidi ya Rais Samia. Hapajengwi kitu,” alisisitiza Ole Kissongo.


Katika hotuba yake, Laigwanani Kissongo aliwasihi vijana wa jamii ya Kimasai kote nchini kuenzi mafunzo waliyopata kipindi cha jando, na kuwa mfano wa maadili mema kwa jamii nzima.


“Tabia hizi zikiachwa zitazalisha kizazi cha hovyo kinachowatukana wakuu wa nchi,” alisema.



Jamii hiyo pia iliomba radhi rasmi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa niaba ya vijana waliokosea, na kumhakikishia Rais Samia kuwa itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kulinda nidhamu, amani na heshima kwa viongozi wa kitaifa.



Mwisho wa mkutano huo mkubwa wa kijadi, uliohudhuriwa na zaidi ya watu 10,000, uliambatana na wito kwa vijana wa jamii hiyo kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, ili kuchagua viongozi wanaowaamini kwa ajili ya maendeleo ya taifa na jamii yao.

0 Comments:

Post a Comment