Kongamano la Pili la Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (NIMCA), lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano (AICC) jijini Arusha, limeandika historia mpya katika tasnia ya habari barani Afrika.
Hotuba zenye uzito na mtazamo wa mbali kutoka kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, pamoja na mfanyabiashara maarufu na mdau wa muda mrefu wa vyombo vya habari, Rostam Azizi, zimeibua mwelekeo mpya wa fikra kuhusu mustakabali wa habari katika enzi za kidijitali.
Akifungua rasmi kongamano hilo kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Dkt. Mpango alisisitiza kuwa hakuna maendeleo ya kweli barani Afrika bila vyombo vya habari huru, vinavyowajibika na vyenye misingi ya taaluma na maadili. Alitoa wito kwa nchi zote za Afrika kuimarisha mifumo ya kisheria na kitaasisi ili kulinda uhuru wa vyombo vya habari na kuendeleza haki ya wananchi kupata taarifa sahihi kwa wakati.
Aliainisha changamoto kubwa inayolikabili bara hili: ongezeko la taarifa potofu na propaganda kupitia mitandao ya kijamii kunakodhoofisha imani ya wananchi kwa vyombo rasmi vya habari. Alieleza kuwa serikali ya Tanzania imeanza mchakato wa mageuzi ya sheria ya habari, ili iendane na katiba, viwango vya kimataifa vya haki za binadamu na matakwa ya zama za kidijitali. Alibainisha pia kuwa Sera mpya ya Habari ipo katika hatua za mwisho, ikilenga kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari huku ikizingatia wajibu na maadili ya taaluma hiyo.
Makamu wa Rais alisisitiza kuwa katika mazingira ya sasa ya teknolojia, hususan matumizi ya akili bandia (AI), kuna haja kubwa ya kuweka miongozo na sheria zitakazolinda matumizi sahihi ya teknolojia hizo katika uandishi na usambazaji wa habari, bila kuhatarisha maadili ya kitaifa na usalama wa kijamii.
Alitoa wito kwa mabaraza ya habari Afrika kuhakikisha kuwa yanajenga mifumo madhubuti ya kushughulikia malalamiko kwa weledi, kutoa mafunzo endelevu kwa waandishi wa habari na kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za taarifa potofu, hasa kwa kutumia teknolojia mpya kwa njia salama na yenye tija.
Katika hotuba yake , Rostam Azizi — mmoja wa waanzilishi wa vyombo vikubwa binafsi vya habari nchini Tanzania — aliweka wazi umuhimu wa kuwekeza katika “miundombinu ya fikra” kwa ajili ya kujenga jamii inayojitambua, inayoheshimu ukweli na inayojenga simulizi zake kwa misingi ya kitaifa na kiafrika.0
Kupitia mjumbe wake Absalom Kibanda, Rostam alirejea historia ya uanzishaji wa vyombo kama Mwananchi Communications na New Habari Corporation, akibainisha kuwa vyombo vya habari si biashara tu, bali ni sehemu ya roho ya taifa; vinapaswa kuwa daraja la mawasiliano kati ya wananchi na mamlaka, na nguzo ya uwajibikaji na maendeleo.
Alionya kuwa mitandao mingi ya kimataifa leo imekuwa chanzo cha taarifa zisizo sahihi kuhusu Tanzania na Afrika kwa ujumla — taarifa ambazo haziangalii maslahi ya wananchi wa bara hili, haziheshimu mila na hazitoi uwajibikaji wowote kwa jamii zinazolengwa.
Kwa maoni yake, suluhisho si kudhibiti uhuru wa habari, bali ni kuwekeza katika majukwaa ya ndani ya kuzalisha na kusambaza habari zenye mizizi ya kitaifa, kwa kutumia teknolojia za kisasa, vijana wabunifu, na waandishi waliobobea katika taaluma.
Alisisitiza kuwa Tanzania haiwezi kuongoza katika maendeleo ya uchumi bila kuongoza pia katika ujenzi wa mifumo ya habari yenye weledi. Alisema kuwa ni wakati wa kuwekeza katika uzalishaji wa taarifa sahihi kama tunavyowekeza kwenye barabara, viwanda na huduma nyingine za msingi, kwa kuwa taarifa ni miundombinu ya fikra na dira ya taifa.
Hotuba hizi mbili zimepokelewa kwa heshima kubwa na washiriki wa kongamano hilo kutoka nchi mbalimbali za Afrika, wakiwemo viongozi wa mabaraza ya habari, wahariri wakuu, watunga sera, wanazuoni na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.
Miongoni mwa hoja zilizojitokeza kwa nguvu katika mkutano huo ni umuhimu wa kulinda uhuru wa vyombo vya habari kwa vitendo, kuimarisha maadili ya taaluma, kujenga mifumo ya mafunzo endelevu kwa waandishi, na kuhakikisha teknolojia kama akili bandia inatumika kuendeleza haki ya wananchi kupata habari — si kuivuruga.
Kongamano hili limefungua ukurasa mpya katika mjadala wa kimkakati kuhusu mustakabali wa habari Afrika. Kwa kauli zao zenye mvuto, Dkt. Mpango na Rostam Azizi wameweka msingi thabiti wa mwelekeo mpya wa uwekezaji, uwajibikaji na ubunifu katika vyombo vya habari vya Afrika, sambamba na ulinzi wa uhuru wa kujieleza na taarifa sahihi katika enzi ya kidijitali.






0 Comments:
Post a Comment