Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa anakabiliwa na mazingira magumu ya kifungo ambayo hayalingani na hali yake ya kisheria, akidai kuwa amekuwa akiwekwa kwenye eneo la wafungwa wa kifo (death row) katika Gereza la Ukonga, licha ya kuwa bado hajahukumiwa kosa lolote.
Akizungumza mbele ya Hakimu Mfawidhi Franco Kiswaga leo Jumatatu, Juni 16, 2025, Lissu alifichua kuwa tangu Ijumaa Kuu, amewekwa kwenye "special room" ya gereza hilo – chumba kinachotumika kuhifadhi wafungwa waliokwishahukumiwa kunyongwa.
"Gerezani, Gereza la Ukonga kuna sehemu moja inaitwa special room, eneo maalum ambalo wanakaa wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kifo kwa kunyongwa. Mimi ninakaa hiyo sehemu wanayokaa wanaosubiri kunyongwa," alisema Lissu.
Akiendelea kueleza hali yake, Lissu alisema kuwa anasindikizwa na askari wawili kila anapotoka kwenda kuonana na mawakili wake au ndugu zake, hali inayofanana kabisa na ile ya wafungwa wa kifo.
"Ninalindwa muda wote, usiku na mchana. Mimi sijahukumiwa kifo lakini ninakaa death row... sasa ukiwa death row, maana yake ni nini?" alihoji Lissu mbele ya Mahakama.
Mbali na malalamiko ya kuwekwa kwenye mazingira hayo, Lissu pia alidai kunyimwa haki ya kuabudu akiwa gerezani.
Katika hatua nyingine ya kushangaza, Lissu aliieleza Mahakama kuwa ameomba rasmi kuwaondoa mawakili wake katika kesi ya uhaini inayomkabili, na kwamba kuanzia sasa atajitetea mwenyewe. Alisema amefikia uamuzi huo kutokana na kutoruhusiwa kuzungumza na mawakili wake kwa faragha kwa zaidi ya siku 68.
"Mawakili wangu walifanya kazi yao kwa ustadi na kwa moyo. Lakini kutokana na mazingira haya ya kutopewa nafasi ya faragha kuwasiliana nao, ninaichukua hii kesi mikononi mwangu. Kuanzia sasa mimi mwenyewe nitakabiliana na mawakili wa serikali," alisema Lissu.
Hakimu Mfawidhi Franco Kiswaga alikubali ombi hilo, na kueleza kuwa Mahakama itamruhusu Lissu kujitetea binafsi hadi pale atakapowasilisha maombi ya kuwarejesha mawakili wake.
"Kwa haya ambayo nimeyasema, mawakili wangu nawashukuru. Walipambana sana, walipigana kitaalamu, mlifanya majukumu yenu na mliyafanya kwa usahihi. Hivyo ninaichukua kesi hii mikononi mwangu tena. Kwahiyo from now on, mimi ndiye nitakaojibizana na hao mawakili wa serikali," alisisitiza Lissu.
Kesi hiyo ya uhaini imeahirishwa hadi Julai 1, 2025, ambapo Lissu anatarajiwa kuanza rasmi kujitetea binafsi dhidi ya mashtaka ya uhaini pamoja na kesi nyingine inayomkabili ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.
Hadi sasa, mashirika ya haki za binadamu na vyama vya kiraia bado hayajatoa tamko rasmi kuhusu madai ya mazingira ya kifungo ya Lissu, ingawa hali hiyo imeibua mjadala mpana kuhusu haki za watuhumiwa na mazingira ya mahabusu nchini.

No comments:
Post a Comment