Saturday, June 7, 2025

Serikali Yaombwa Kuwezesha KARIBU-KILIFAIR kwa Kulitangaza Rasmi Eneo la Maonesho Arusha kuwa Kituo cha Kimataifa

 



Mkurugenzi wa KARIBU-KILIFAIR, Dominic Shoo, ametoa wito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuongeza uwekezaji katika masoko ya kimataifa, kutoa msaada wa kifedha kwa maonesho hayo na kuboresha miundombinu ya eneo la maonesho jijini Arusha, kwa kulifanya kuwa eneo rasmi la kudumu la maonesho ya kimataifa.

Tunaomba serikali iwekeze zaidi kwenye masoko ya kimataifa, itoe msaada wa kifedha wa moja kwa moja, na kutangaza eneo hili la maonesho kama ‘International Standard Event Ground’ ya kudumu. Hii itakuwa hatua kubwa ya kulitangaza taifa letu,” alisisitiza Shoo mbele ya viongozi wa serikali, wadau wa utalii na washiriki kutoka mataifa mbalimbali.

Shoo alisema kuwa kuwepo kwa kituo cha kudumu chenye hadhi ya kimataifa kutaiwezesha Tanzania kuandaa maonesho makubwa ya kitalii kila mwaka, jambo ambalo litasaidia kuongeza idadi ya watalii, wawekezaji na kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta ya utalii.

Maonesho haya ni zaidi ya tukio la kibiashara. Ni jukwaa la kitaifa na kikanda la fahari ambalo linahitaji miundombinu ya kisasa, maji safi, umeme wa uhakika, maabara za uhakiki wa bidhaa na huduma nyingine muhimu za kimataifa,” alieleza Shoo.

Ameongeza kuwa KARIBU-KILIFAIR imejipambanua kama jukwaa kuu la utalii barani Afrika, likiwa na uwezo mkubwa wa kufikia masoko ya kimataifa, kuvutia wanunuzi wa huduma za utalii, na kujenga taswira chanya ya Tanzania kama kitovu cha utalii endelevu na wa kisasa.

Kwa msaada na ushirikiano wa Serikali yetu, na chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunaamini Tanzania siyo tu itaendelea kuongoza Afrika, bali pia kuwa kitovu cha utalii, biashara na ubunifu duniani,” alisema Shoo kwa matumaini makubwa.

Kauli hiyo ya Shoo imeungwa mkono na wadau wengi wa sekta ya utalii waliokuwepo katika hafla hiyo ya uzinduzi wa KARIBU-KILIFAIR 2025, wakisisitiza kuwa uwekezaji wa kimkakati kutoka serikalini ndio utakaoifanya Tanzania kuwa mwenyeji wa maonesho ya kiwango cha kimataifa kwa miaka mingi ijayo.

Maonesho ya mwaka huu yanajumuisha washiriki zaidi ya 500 kutoka mataifa 13 na wanunuzi wa huduma kutoka zaidi ya nchi 40, yakiwa na lengo la kuendeleza ushirikiano wa kikanda na kimataifa, pamoja na kukuza sekta ya utalii kama injini ya uchumi wa taifa.

No comments:

Post a Comment