Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwathamini na kuwajali watu wenye ulemavu, wakiwemo wenye ualbino, kwa kuhakikisha wanapata ulinzi na fursa stahiki katika ujenzi wa Taifa.
Akizungumza leo Ijumaa, Juni 13, 2025, katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Uelewa kuhusu Ualbino yaliyofanyika katika uwanja wa Mwanga Centre, Kigoma, Majaliwa amesema:
“Serikali itaendelea kuchukua hatua mahsusi za kuimarisha ustawi na utoaji huduma kwa watu wenye ualbino ikiwemo kuwatambua, kuimarisha mifumo ya kisera na kuwezesha upatikanaji wa huduma muhimu hapa nchini.”
Amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kutumia mikopo inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri. Hadi kufikia Machi 2025, jumla ya shilingi bilioni 5.48 zimetolewa kwa vikundi 891 vya Watu Wenye Ulemavu nchini.
Aidha, amesema kuwa Serikali imeongeza ruzuku kwa vyama vya Watu Wenye Ulemavu hadi shilingi milioni 230 kwa mwaka 2024/2025 kutoka shilingi milioni 200 zilizotolewa mwaka uliopita.
“Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali ilitenga shilingi bilioni 8.743 kwa ajili ya huduma za ustawi wa Jamii na shilingi milioni 182.8 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta kinga ya saratani ya ngozi kwa watu wenye Ualbino.”
Ameongeza kuwa tangu Julai 2021 hadi Juni 2024, Serikali kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ilitumia zaidi ya shilingi milioni 500 kusambaza mafuta hayo katika mikoa yote 26 ya Tanzania.
Waziri Mkuu pia aliwaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Haki na Ustawi kwa Watu wenye Ualbino, Mkakati wa Taifa wa Teknolojia Saidizi na Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Taarifa za Watu wenye Ulemavu (PD-MIS).
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, alisema:
“Kupitia maadhimisho haya, Serikali imezindua programu janja ‘Albino Mobile App’ ambayo itawezesha kufanya usajili na ukusanyaji wa taarifa za watu wenye ualbino kwa njia ya kidigitali.”
“Mfumo huu utapunguza gharama za usafiri na usafirishaji wa vifaa kwa ajili ya usajili, na pia kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi zinazosaidia Serikali kupanga na kutekeleza sera kwa ufanisi.”
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS), Godson Mollel, aliipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali ilizochukua kusaidia kundi hilo.
“Serikali imefanya mambo makubwa yenye lengo la kuwawezesha watu wenye albino nchini ikiwemo kutoa fedha kwa ajili ya kununua mafuta kinga ambayo hugawiwa bure.”
“Pia, Serikali imetoa agizo kwa halmashauri kutoa fedha kwa ajili ya kununua mafuta kinga ambayo imesaidia kupunguza uhaba wa mafuta kinga.”
Godson pia aliwataka watu wenye ulemavu kushiriki kwa wingi katika uchaguzi mkuu ujao.
“Jitokezeni kwa wingi kushiriki katika uchaguzi mkuu, mkifanya hivyo mtakuwa mmetimiza haki yenu ya kikatiba ya kuchagua au kuchaguliwa.”
Katika maadhimisho hayo, Waziri Mkuu alizindua rasmi programu ya kidigitali ya usajili ya watu wenye ualbino – Albino Mobile App – kwa lengo la kuwawezesha kusajiliwa na kutambuliwa kwa usahihi katika mfumo wa Serikali.


No comments:
Post a Comment