Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi kiwanda cha uzalishaji wa mbolea cha ITRACOM Fertilizers Ltd kilichopo Nala, jijini Dodoma tarehe 28 Juni 2025.
Uzinduzi huo utahusisha uwekaji wa jiwe la msingi, upandaji miti kama ishara ya kuhifadhi mazingira na kuhimiza kilimo endelevu, pamoja na ukaguzi wa miundombinu ya kisasa ya kiwanda hicho. Hafla hiyo ya kihistoria inatarajiwa kuhudhuriwa na Marais wa nchi jirani akiwemo Rais wa Jamhuri ya Burundi, Meja Jenerali mstaafu Evariste Ndayishimiye, pamoja na Viongozi Wakuu wa Serikali, wakiwemo Mawaziri wa Kilimo kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na wananchi wa Dodoma na mikoa ya jirani.
Akizungumza na waandishi wa habari tarehe 11 Juni 2025 kuelekea uzinduzi huo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema, “Kaulimbiu ya hafla hiyo ni ‘Kilimo ni Mbolea na Mbolea ni FOMI’.” Alisema kuwa kiwanda cha ITRACOM ni matokeo ya uwekezaji mkubwa ulioanza mwaka 2021, kikilenga kuongeza uzalishaji wa mbolea ndani ya nchi, kupunguza utegemezi wa uagizaji wa mbolea kutoka nje, na kuunga mkono juhudi za serikali za kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.
Waziri Bashe alieleza kuwa kiwanda hicho tayari kimeajiri wafanyakazi wapatao 1,805 huku ajira zisizo za moja kwa moja zikikadiriwa kuwa zaidi ya 5,000. Aliongeza kuwa matarajio ya baadaye ni kufikia zaidi ya ajira 3,000 za moja kwa moja na ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 15,000.
“Ujenzi wa kiwanda ulianza mwaka 2021 na kina uwezo wa kutengeneza aina mbalimbali za mbolea kulingana na udongo na aina ya mazao. Hadi sasa kimeshasajili aina 14 za mbolea zinazotumika kwa mazao yote yanayolimwa nchini,” alisema Bashe. Aliongeza kuwa kiwanda hicho pia huzalisha chokaa-kilimo kwa ajili ya kurekebisha udongo ulioathiriwa na tindikali.
Kuhusu mbolea zinazozalishwa, Bashe alisema kuwa “Mbolea za Fomi Otesha, Fomi Kuzia na Fomi Nenepesha zilianza kuingia sokoni mwezi Desemba 2022. Mbolea hizi hutumika kuboresha afya ya udongo na kuongeza mavuno kwenye mazao ya chakula na biashara.”
Katika kuhakikisha kuwa viwanda vya ndani vinapata soko la uhakika, serikali imepanga kununua tani 200,000 za mbolea pamoja na tani 50,000 za chokaa kutoka viwanda vya ndani. Bashe alisisitiza kuwa hatua hiyo haitavuruga mfumo wa ruzuku uliopo.
“Tutanunua mbolea kutoka viwanda vya ndani na kupeleka kwenye maeneo ambayo mbolea hazitumiki sana ili Watanzania waanze kuzitumia na kuona matokeo yake,” alisema. Aidha, alieleza kuwa kwa sasa Tanzania ilikuwa ikiagiza hadi tani milioni 1.2 za mbolea kutoka nje ya nchi, lakini uwepo wa kiwanda cha ITRACOM na uwekezaji mwingine unaoendelea unalenga kupunguza uagizaji huo kwa kiasi kikubwa.
Waziri Bashe aliwataka wananchi wa Dodoma na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uzinduzi huo wa kihistoria na kuunga mkono juhudi za serikali za kuinua sekta ya kilimo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kiwanda cha ITRACOM Fertilizers Ltd, Nazaire Nduwimana, alisema kuwa kiwanda hicho kinazalisha mbolea kwa kushirikiana na taasisi za serikali kama Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).
“Mpaka sasa tunazalisha aina 14 za mbolea. Kiwanda chetu kina uwezo wa kuzalisha mbolea kulingana na eneo, zao na hata hitaji la mkulima,” alisema Nduwimana. Aliongeza kuwa mbolea zinazozalishwa zinatumia mchanganyiko wa chumvi chumvi pamoja na malighafi za asili kama samadi na nyinginezo, jambo linalolenga kuongeza tija na kuimarisha afya ya udongo.
Uzinduzi wa kiwanda hiki unakuja miaka mitatu na nusu tangu uwekezaji kuanza kutekelezwa jijini Dodoma, na unatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo nchini Tanzania.



No comments:
Post a Comment