Dar es Salaam – Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imetoa zuio la muda kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), likiwazuia kufanya shughuli zozote za kiutendaji na oparesheni hadi kesi ya msingi iliyofunguliwa dhidi ya chama hicho itakaposikilizwa.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Hamidu Mwanga anayesikiliza kesi namba 8323/2025, kufuatia maombi yaliyowasilishwa na Mawakili wa waleta maombi wakiongozwa na Wakili Gido Thomas Simfukwe. Walalamikaji katika kesi hiyo ni aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Saidi Issa Mohamed pamoja na wenzake wawili.
Jaji Mwanga amesema kuwa: "Suala hili ni la kisheria na haliitaji ubishani kwa sababu limefafanuliwa vyema kwenye sheria ya vyama vya siasa."
Katika kesi ya msingi inayotarajiwa kuanza kusikilizwa Juni 24, 2025, waleta maombi wanadai kuwa CHADEMA imekuwa ikiitenga Zanzibar katika masuala mbalimbali ya kichama, ikiwemo mgawanyo wa rasilimali kama fedha.
Katika hatua ya kushangaza, upande wa utetezi kutoka CHADEMA haukuwakilishwa Mahakamani baada ya Wakili Jebra Kambole kujiondoa katika kesi hiyo. Kutokana na hilo, Mahakama iliendesha shauri hilo upande mmoja pekee.
Kwa mujibu wa uamuzi huu, shughuli zote za ndani za chama hicho zikiwemo mikutano ya hadhara, vikao vya chama, na oparesheni nyingine, zimezuiliwa kwa muda hadi pale kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Taarifa zaidi kuhusu mwenendo wa shauri hili zitasubiriwa baada ya tarehe 24 Juni, 2025.

0 Comments:
Post a Comment