Kijana Aokolewa Baada ya Kujitupa Baharini Kutokea Katika Boti

  


Katika tukio la kushtua lililotokea Juni 17, 2025, kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Muhammed Shaib Saleh (35), mkazi wa Mbuyuni, Pemba, amenusurika kufa baada ya kujirusha baharini akiwa ndani ya boti ya mwendo kasi ya Zan Fast Ferries. 


Boti hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Bandari ya Mkoani, Pemba kuelekea Bandari ya Malindi, Unguja.

Kwa mujibu wa taarifa, tukio hilo lilitokea majira ya saa nane mchana, kijana huyo alijitupa baharini katika mkondo wa bahari ya Nungwi. Mabaharia wa boti hiyo walichukua hatua za haraka kwa kuzima injini na kurusha vifaa vya uokozi, hatua iliyochangia kumuokoa kijana huyo ndani ya dakika 10.

Nahodha wa boti hiyo, Muhamed Khamis, amesema:

"Tulipoona kijana amejirusha, tulizima injini mara moja na tukarusha vifaa vya uokozi, tukafanikiwa kumtoa majini akiwa hai."

Baadhi ya mashuhuda waliokuwemo ndani ya boti hiyo wamesema kuwa kabla ya tukio hilo, kijana huyo alikuwa akiulizia mara kwa mara kama wamefika Nungwi.

Rashid Sultani, mmoja wa mashuhuda, amesema:

"Kijana hakuwa anaonekana kama ana matatizo ya akili, sijui alipatwa na nini hadi akachukua uamuzi wa kujitupa baharini."

Baada ya kuokolewa, Muhammed alikabidhiwa kwa askari wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi, huku hali yake ikiripotiwa kuwa nzuri.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), Mtumwa Said, amesema:

"Uwepo wa vifaa vya kisasa vya uokozi umechangia kuokoa maisha ya kijana huyo."

Boti ya Zan Fast Ferries huondoka Pemba majira ya saa saba mchana na huchukua takribani saa tatu kufika Unguja, ikiwa ni moja ya njia muhimu za usafiri baharini kati ya visiwa hivyo viwili.

Chanzo: Nipashe Digital

0 Comments:

Post a Comment