Mkoa wa Arusha unaendelea kuwa kitovu cha mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii huku serikali ya awamu ya sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiweka mkazo maalum katika kukuza sekta ya utalii na kuimarisha miundombinu kama njia ya kuufungua mkoa huo kwa fursa pana zaidi za maendeleo.
Katika kikao cha pamoja na viongozi kutoka Shirika la Reli Tanzania na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Christian Makonda, amesema kuwa nia ya Rais Samia ni kuifanya Arusha kuwa lango kuu la uchumi kupitia matumizi ya rasilimali zilizopo, hasa kwenye sekta ya utalii ambayo tayari inauwezo mkubwa wa kuvutia wageni na kuingiza mapato makubwa.
“Ndoto ya Rais Samia kwa Arusha ni kuona mkoa huu unakuwa kitovu cha utalii na uchumi. Hilo ndilo tunalolishuhudia sasa kupitia miradi mikubwa ya ujenzi wa uwanja wa kisasa na ukumbi wa mikutano, ambayo inalenga kuvutia wageni na wawekezaji,” alisema Makonda.
Ameeleza kuwa hatua ya Rais kuwatuma viongozi wa mashirika ya kimkakati kama reli na bandari ni ishara ya dhamira ya kweli ya serikali kuhakikisha maendeleo hayo yanafika kwa wananchi kwa haraka na kwa tija.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Reli Tanzania, Ally Karavina, amesema kuwa wameona umuhimu wa kuboresha reli ya kutoka Arusha hadi Dar es Salaam kwa kuifufua na kuifikiria kwa mtazamo mpana zaidi hadi Tanga, ili kurahisisha shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo.
“Tayari tumeanza mradi wa ukarabati wa reli hiyo, na lengo ni kuhakikisha treni zinaweza kusafiri kwa kasi ya wastani wa kilomita 70 kwa saa. Yanayokuja Arusha yanaridhisha. Mpango wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR bado upo kama ulivyoainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, na reli hiyo itarahisisha usafirishaji wa magadi soda kutoka Engaruka hadi Musoma,” alisema Karavina.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Plusduce Mbosaa, alitoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi kuchangamkia fursa ya ujenzi wa Bandari Kavu jijini Arusha, akisema kuwa tayari taasisi hiyo iko tayari kutoa vibali kwa mtu au taasisi yoyote yenye nia ya kuwekeza katika mradi huo.
“Mizigo yote itakayopokelewa kupitia bandari ya Arusha itapitia katika bandari kavu hiyo, hatua itakayorahisisha shughuli za usafirishaji na kuongeza ufanisi katika biashara. Ni fursa ambayo kila mfanyabiashara anatakiwa kuitumia kikamilifu,” alisema Mbosaa.
Uwekezaji huu katika sekta za usafiri na usafirishaji unatajwa kuwa chachu muhimu ya kuimarisha uchumi wa mkoa wa Arusha, si tu kwa kukuza utalii bali pia kwa kufungua mkoa huo kuwa kitovu cha biashara na huduma kwa mikoa jirani na nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa ujumla, jitihada hizi zinaonyesha mwelekeo wa serikali wa kuhakikisha Arusha inatumia kikamilifu rasilimali zake za kipekee ili kujenga uchumi imara, jumuishi na endelevu unaowanufaisha wananchi kwa kiwango kikubwa.
▼

No comments:
Post a Comment