Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, amezindua rasmi soko la kisasa la nyama choma katika eneo la Kumbilamoto, Vingunguti, wilayani Ilala jijini Dar es Salaam. Uzinduzi huo umeambatana na utiaji saini wa mikataba ya utekelezaji wa miradi sita ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 7.7.
Soko hilo, ambalo limejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 727, linatarajiwa kuwa chanzo kikubwa cha ajira na kipato kwa wakazi wa jiji hilo, hususan wanawake na vijana.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mchengerwa alipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa usimamizi mzuri wa mradi huo na kusisitiza kuwa ni mfano bora wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaopaswa kuigwa na halmashauri nyingine nchini.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri. Halmashauri nyingine nchini zinapaswa kuiga mfano huu. Soko hili la kisasa litatoa fursa nyingi za ajira na kukuza uchumi wa wananchi. Ni muhimu likatunzwa vizuri ili lisiharibike mapema,” alisema Mchengerwa.
Aidha, alieleza kuwa ujenzi wa soko hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), akibainisha kuwa serikali ya awamu ya sita tayari imefanikiwa kutekeleza miradi mingi ya kimkakati kama ilivyoahidi.
“Kukamilika kwa mradi huu ni ushahidi wa dhamira ya kweli ya serikali ya awamu ya sita. Miradi mingi imekamilika nchini kote, na hii inaonyesha kuwa ahadi zilizotolewa zinatekelezwa kwa vitendo,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Mchengerwa alizitaka halmashauri zote kuhakikisha zinatekeleza kikamilifu malengo ya ukusanyaji mapato ili kuweza kufanikisha miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
“Mapato ni msingi wa maendeleo. Halmashauri zetu zibuni miradi bunifu yenye tija, na zitimize malengo ya mapato ili kuendelea kuwahudumia wananchi kwa ufanisi,” alisema.
Pia alisisitiza umuhimu wa kuwapa kipaumbele wakandarasi wazawa katika miradi ya maendeleo na kuonya dhidi ya wakandarasi wasiowajibika.
“Ni wakati wa kuwapa nafasi wakandarasi wazawa, lakini wale watakaoshindwa kutekeleza miradi kwa viwango vinavyotakiwa wachukuliwe hatua stahiki,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogole, alimhakikishia waziri kuwa miradi yote iliyosainiwa itakamilika kabla ya mwisho wa mwaka na kuwa wananchi watanufaika moja kwa moja na matokeo yake.
“Tunaahidi kukamilisha miradi yote kabla ya mwisho wa mwaka huu. Wananchi wa Ilala watashuhudia matokeo chanya kupitia utekelezaji huu,” alisema Mpogole.
Naye Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu, alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kudumisha amani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
“Natoa wito kwa Watanzania wote kuepuka vitendo vya kuvunja amani. Uchaguzi ni haki ya kidemokrasia, tusiruhusu tofauti za kisiasa kuvuruga mshikamano wetu,” alisema Zungu.
Katika upande wa wanufaika wa soko hilo, mfanyabiashara Amina Selemani alieleza furaha yake na kutoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha mradi huo.
“Tunamshukuru sana Rais wetu kwa kutuletea mradi huu wa soko. Umekuwa ukombozi mkubwa kwa maisha yetu, hasa sisi kina mama,” alisema Amina.




0 Comments:
Post a Comment