Tuesday, May 27, 2025

WANAOKIUKA MARUFUKU YA MIFUKO YA PLASTIKI KUKIONA


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa onyo kali kwa watu binafsi na kampuni zinazokaidi marufuku ya uzalishaji na matumizi ya mifuko ya plastiki kwa kuendelea kuzalisha, kuingiza na kusambaza bidhaa hizo kwa njia zisizo halali.




Onyo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, leo Mei 27, 2025 jijini Dodoma, alipokuwa akitoa tamko rasmi la Serikali kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani. Waziri Masauni amesema Serikali imejipanga kufanya doria za kushtukiza katika maeneo mbalimbali ikiwemo viwandani, masokoni na kwenye viwanda bubu ili kuwabaini na kuwachukulia hatua kali wote wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.

“Itaendelea kufanyika doria za kushtukiza katika viwanda, viwanda bubu na masoko ili kuwabaini na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaokiuka marufuku hii,” amesema Mhandisi Masauni.

Ameeleza kuwa licha ya kuwepo marufuku ya mifuko ya plastiki tangu mwaka 2019, bado baadhi ya watu wamekuwa wakitumia ujanja wa kutumia vifungashio vya plastiki aina ya tubings kama vibebeo—hatua ambayo si tu ni kinyume cha sheria, bali pia ni hatari kwa mazingira. Vifungashio hivyo havikidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Akitilia mkazo kuhusu hatua zitakazochukuliwa, Waziri Masauni amezielekeza taasisi za Serikali zikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi nyingine za umma kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria na kanuni dhidi ya matumizi ya plastiki.

“Niwakumbushe Watanzania wenzangu kuzingatia maelekezo ya Serikali kuachana na mifuko ya plastiki na kutumia mifuko mbadala ambayo kwa sasa inapatikana nchini kote kwa gharama nafuu,” amesisitiza Mhandisi Masauni.

Waziri huyo amesema licha ya changamoto hiyo, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kudhibiti taka za plastiki tangu marufuku hiyo ilipoanza kutekelezwa rasmi Juni 2019, hatua ambayo imechangia kupunguza kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira.

“Pamoja na changamoto zilizopo, kwa kiasi kikubwa Tanzania imepiga hatua katika kudhibiti taka za plastiki baada ya kupiga marufuku uzalishaji, uingizaji, usambazaji na matumizi ya mifuko ya plastiki kuanzia Juni, 2019,” amesema Waziri Masauni.

Katika kuhakikisha wananchi wanaelewa mifuko ipi inaruhusiwa na ipi hairuhusiwi, Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa umma kwa kushirikiana na sekta binafsi, lengo likiwa ni kuhakikisha mifuko mbadala rafiki kwa mazingira inapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu.

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani

Akizungumzia kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu, Waziri Masauni amesema kilele cha maadhimisho hayo kitaadhimishwa jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Maadhimisho hayo yataambatana na maonesho ya bidhaa, huduma na ubunifu kuhusu hifadhi ya mazingira kuanzia Juni 1 hadi 5, 2025.

Aidha, kutakuwa na Kongamano la Vijana litakalofanyika Juni 3, 2025 jijini Dar es Salaam, ambalo litawakutanisha vijana kutoka vyuo vikuu, wajasiriamali pamoja na mabalozi wa mazingira.

Kwa mwaka huu, maadhimisho haya yanaongozwa na kaulimbiu:
"Tanzania Ijayo Tuwajibike Sasa, Dhibiti Matumizi ya Plastiki"
Kaulimbiu hii inalenga kuikumbusha jamii kuwa mazingira ni msingi wa maisha, afya ya jamii, na uchumi wa taifa. Kwa mantiki hiyo, uhifadhi na utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila Mtanzania.

Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wote wanaokaidi sheria kwa kusambaza au kutumia mifuko ya plastiki, huku ikiendelea kutoa elimu na kuhamasisha matumizi ya mbadala bora na salama kwa mazingira ya nchi yetu.

No comments:

Post a Comment