Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limeomba uchunguzi wa haraka na wa wazi kuhusu tukio la kuvamiwa na kujeruhiwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Padre Charles Kitima, lililotokea usiku wa tarehe 30 Aprili 2025 katika Makao Makuu ya TEC yaliyopo Kurasini, Temeke – Dar es Salaam.
Katika taarifa rasmi kwa umma iliyotolewa na TEC, Baraza limesema tukio hilo ni la kusikitisha na la kinyama, na linahitaji kushughulikiwa kwa haraka ili kurejesha imani kwa wananchi. "Padre Kitima alipata majeraha makubwa na amelazwa katika hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam," imeeleza taarifa hiyo.
TEC imeeleza kuwa tayari Serikali na vyombo vya usalama vimeonyesha ushirikiano mzuri, lakini ikaongeza kuwa "Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kuchukua hatua za haraka za kuwabaini na kuwakamata wale wote waliohusika katika kupanga na kutekeleza uhalifu huu wa kinyama na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria."
Aidha, TEC imetoa rai kwa vyombo husika kutoa taarifa sahihi na kwa uwazi kwa umma kuhusu maendeleo ya uchunguzi ili kuondoa upotoshaji na kuweka wazi ukweli wa tukio hilo. Baraza pia limewashukuru wote waliomsaidia Padre Kitima kufikishwa hospitalini na wanaoendelea kumuhudumia.
"Tunaomba Waamini na watu wenye mapenzi mema muendelee kumuombea neema ya uponyaji Padre Kitima, na pia kuliombea Taifa letu amani na umoja," amesema Askofu Eusebius Nzigilwa, Makamu wa Rais wa TEC, katika taarifa hiyo ya Mei 1, 2025.
Kwa upande mwingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam nalo limetoa taarifa ya awali kuhusu tukio hilo, likieleza kuwa tukio hilo liliripotiwa rasmi majira ya saa nne usiku wa tarehe 30 Aprili 2025.
Kwa mujibu wa Polisi, Padre Kitima alihudhuria kikao na viongozi wa dini mbalimbali kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa moja jioni, kisha alielekea kwenye kantini ya Baraza hilo na kuendelea kupata kinywaji hadi saa nne na robo usiku.
Akiwa njiani kuelekea maliwatoni, alishambuliwa kichwani kwa kitu butu na watu wawili wasiojulikana.
"Alipelekwa hospitali ya Aga Khan na anaendelea vizuri na matibabu. Mtu mmoja Rauli Mahabi @Haraja, mkazi wa Kurasini, anashikiliwa na kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo," imesema taarifa ya Jeshi la Polisi.
Polisi wameeleza kuwa uchunguzi wa kina unaendelea na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika. Wananchi wametakiwa kuwa na utulivu wakati uchunguzi unaendelea.



0 Comments:
Post a Comment