
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ameshuhudia utiaji saini wa hati ya makubaliano ya ujenzi wa kituo kikubwa cha upandikizaji figo ambacho kinatarajiwa kuwa kikubwa zaidi katika Ukanda wa Jangwa la Sahara. Kituo hicho kitajengwa katika Hospitali ya Kanda ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma, kwa ushirikiano kati ya Shirika la Tiba la TOKUSHUKAI (Japan), Hospitali ya Benjamin Mkapa, na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Makubaliano hayo yalisainiwa jana, Mei 26, 2025, katika kongamano la Biashara, Uwekezaji na Utalii lililofanyika Hoteli ya Westin, Osaka, Japan, ikiwa ni sehemu ya ushiriki wa Tanzania katika maonyesho ya World Expo Osaka 2025. Kongamano hilo lilifunguliwa rasmi na Waziri Mkuu Majaliwa.
Akizungumza baada ya utiaji saini, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi, alisema:
“Hawa ni wadau wetu wa muda mrefu na walikuwa watu wa kwanza kusaidia utoaji wa huduma za Dialysis katika hospitali ya Benjamin Mkapa. MOU hii ambayo tumeisaini sasa hivi ni kwa ajili ya kujenga kituo cha umahiri katika upandikizaji figo kwenye eneo la Tanzania na Ukanda wa Jangwa la Sahara.”
Prof. Makubi aliongeza kuwa mradi huo utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 28, ikiwa ni msaada kutoka kwa TOKUSHUKAI bila masharti yoyote, na unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu.
“Tunatoa shukurani kwa Serikali ya Japan kupitia wadau hao na tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi ambayo yametufanya sisi tuweze kufikia makubaliano haya. Makubaliano haya yanakwenda kusaidia wananchi kwa ajili ya kuboresha huduma za figo si kwa Watanzania tu bali kwa Waafrika wengine,” alisema Profesa Makubi.
Mbali na kutoa huduma za kupandikiza figo, kituo hicho pia kitatoa mafunzo na kufanya tafiti zinazolenga kuzuia na kupunguza magonjwa ya figo, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Lugano Kusiluka, alisema:
“Makubaliano haya yataimarisha huduma ya upandikizaji figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa. Kwa sasa tupo katika mchakato wa kuanzisha programu ya uhandisi wa vifaa tiba ili kuounguza gharama kwa Serikali kutumia wataalam kutoka nje ya nchi kutengeneza vifaa hivyo mara vinapoharibika.”
Aidha, Prof. Kusiluka alibainisha kuwa kituo hicho kitakuwa na nafasi kubwa ya kimataifa katika kutoa mafunzo kwa madaktari bingwa na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, si tu kwa ajili ya upandikizaji wa figo, bali pia baadaye kwa viungo vingine.
Pia, hati nyingine ya makubaliano ilisainiwa kati ya Chuo Kikuu cha Dodoma, Hospitali ya Benjamin Mkapa, na Chama cha Maendeleo na Uchumi Afrika cha Japan (AFRECO), ikiwa ni sehemu ya jumla ya hati sita zilizosainiwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na mashirika mbalimbali ya Japan.
Makubaliano haya yanatarajiwa kuimarisha zaidi mfumo wa afya nchini na kuiweka Tanzania kwenye ramani ya Afrika kama kitovu cha huduma za kibingwa za figo.
0 Comments:
Post a Comment