Serikali Yalaani Shambulio la Padre Kitima, Yasihi Kudumisha Amani Kabla ya Uchaguzi

 


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, amesema Serikali inalaani vikali na kukemea tukio la kushambuliwa na kuumizwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padre Dkt. Charles Kitima, pamoja na matukio mengine yote ya uvunjifu wa sheria.



Akizungumza wakati wa Misa ya kumsimika Askofu wa Jimbo Jipya Katoliki la Bagamoyo, Mhashamu Askofu Stephano Lameck Musomba, iliyofanyika katika Uwanja wa St. Mary Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani, Dkt. Mpango alisema:
“Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani imeviagiza vyombo vya dola kuwatafuta, kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria wahusika wa tukio hilo, na wale wote watakaothibitika kuhusika na matukio kama hayo.”


Amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu wakati wa maandalizi na kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu, akionya dhidi ya matumizi ya lugha za chuki na uchochezi.

“Ni vema kuepuka kauli za kibaguzi, kichochezi, uzushi na upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii na njia nyingine za mawasiliano kwa misingi ya tofauti ya itikadi za kisiasa, kidini, kabila au rangi,” alisema.

Makamu wa Rais aliwaasa vijana kutotumiwa na wanasiasa wachochezi:
“Vijana msikubali kutumiwa na wanasiasa wenye uchu wa madaraka walio tayari kuwatumia kuchochea vurugu kwa manufaa yao binafsi.”

Amesisitiza pia kuwa ni jukumu la watendaji wa serikali kutenda haki kwa mujibu wa sheria na maadili ya utumishi wa umma.

“Watendaji Serikalini tunapaswa kutenda haki katika utekelezaji wa majukumu yetu,” aliongeza.

Katika hotuba yake, alieleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini ili kuhakikisha taasisi za kidini zinaendelea kutoa huduma kwa jamii.
“Serikali inathamini mchango mkubwa wa Kanisa Katoliki na madhehebu mengine ya dini katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii, hususan afya na elimu,” alisema.

Akizungumzia uzinduzi wa Jimbo Jipya la Bagamoyo, Dkt. Mpango alisema:
“Uamuzi wa Baba Mtakatifu Francis kuunda Jimbo jipya la Bagamoyo si tu umeipa Bagamoyo hadhi, bali pia umesogeza huduma za kichungaji kwa waamini na utaongeza kasi ya uinjilishaji.”

Vilevile, alitoa salamu na pongezi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa wanajimbo la Bagamoyo kwa kupata Jimbo na Mchungaji Mkuu mpya.

“Bagamoyo imekuwa ndiyo mlango wa kuingia kwa imani ya Kikristo hapa nchini na maeneo mengine ya Afrika Mashariki na Kati,” alisema.

0 Comments:

Post a Comment