Katibu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dkt. Charles Kitima, ameripotiwa kushambuliwa na watu wasiojulikana akiwa katika makazi yake ndani ya ofisi za TEC, eneo la Kurasini jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia Aprili 30, 2025.
Kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwepo katika mgahawa mmoja ndani ya viunga vya TEC, Padri Kitima alionekana akiwa katika mazungumzo na baadhi ya watu kabla ya kuinuka kuelekea msalani. Dakika chache baadaye, watu wasiojulikana walitokea ghafla na kumshambulia kwa muda mfupi kisha kutoweka mara moja.
Baada ya tukio hilo, Padri Kitima alikutwa akivuja damu sehemu mbalimbali za mwili na kuomba msaada. Alipatiwa huduma ya kwanza katika kituo kidogo cha afya kilichopo ndani ya eneo hilo kabla ya kusaidiwa kupandishwa kwenye gari na kupelekwa hospitalini kwa matibabu zaidi. Hadi taarifa hii inaandaliwa, bado haijafahamika rasmi hospitali alikokimbizwa.
Padri Kitima ni mmoja wa viongozi mashuhuri wa Kanisa Katoliki nchini, na amekuwa mstari wa mbele katika kupaza sauti dhidi ya ukandamizaji wa haki, ukiukwaji wa sheria, na katika kupigania demokrasia na haki za binadamu. Umaarufu wake katika kuzungumzia masuala ya kijamii na kisiasa umemfanya kuwa sauti yenye ushawishi mkubwa katika jamii ya Watanzania.
Tukio hilo limelaaniwa vikali na watu mbalimbali mashuhuri nchini, wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, wanaharakati na wanasheria.
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, John Heche, ameandika kwenye ukurasa wake wa X:
"Nimepokea taarifa mbaya za kushambuliwa kwa Mwalimu wangu Dr Kitima usiku huu.
Hii ni habari mbaya sana kwa nchi yetu, tumefikaje hapa?
Get well soon Father, tunakuombea."
Wakili Jebra Kambole naye ameandika:
"Get well soon Father Dr. Charles Kitima! Shambulio dhidi yako, ni shambulio dhidi ya wapigania haki!!! Hatuko salama!!!"
Wakili Paul Kisabo amesema:
"Pole sana Padri Kitima, alaaniwe mtu yule aliyekushambulia."
Kwa upande wake, Dawson Kagine ameandika kwa masikitiko:
"Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya kushambuliwa kwa Fr. Kitima. Namuombea kwa Mwenyezi Mungu apone haraka."

0 Comments:
Post a Comment