Safari zote za ndege zilisitishwa kwa muda katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Roberts (RIA) usiku wa Alhamisi baada ya ndege ya kibinafsi iliyombeba Rais wa Liberia, Joseph Boakai, kupata hitilafu ya kiufundi na kulazimika kutua kwa dharura.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Liberia (LCAA), sehemu ya gia ya kutua ya ndege hiyo iliharibika wakati ilipokuwa ikikaribia kutua uwanjani hapo. Tukio hilo liliibua hali ya taharuki miongoni mwa wafanyakazi wa uwanja wa ndege na abiria waliokuwa wakisubiri safari zao.
Rais Boakai alikuwa akirejea kutoka ziara rasmi nchini Nigeria pamoja na wasaidizi wake kadhaa. Mamlaka zimeripoti kuwa hakuna mtu aliyejeruhiwa na wote waliondolewa salama katika eneo la tukio.
Kutokana na tukio hilo, safari zote za ndege zilizopangwa kufanyika usiku huo ziliahirishwa kwa muda ili kutoa nafasi kwa uchunguzi na kuondoa ndege hiyo kutoka katika njia ya kurukia.
Picha za ndege hiyo ikiwa imekwama zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, na kuzua mijadala kuhusu hali ya usalama wa anga nchini Liberia.
Hadi sasa, haijafahamika ikiwa ndege hiyo ni mali ya serikali au ni ya kukodiwa, lakini msemaji wa Ikulu ya Liberia ameahidi kutoa taarifa kamili baada ya uchunguzi kukamilika.


0 Comments:
Post a Comment