Mwanamfalme Harry: "Ningependa Maridhiano, Maisha Ni ya Thamani"



Duke wa Sussex, Mwanamfalme Harry, amesema angetamani kuwepo kwa maridhiano kati yake na Familia ya Kifalme ya Uingereza, huku akifichua maumivu na masikitiko yake kufuatia kushindwa kwake kwenye kesi ya rufaa kuhusu usalama wake akiwa nchini Uingereza.



Akizungumza kwa hisia katika mahojiano na BBC News yaliyofanyika California, Harry alisema:

“Ningependa maridhiano na familia yangu. Hakuna maana kuendelea kupigana tena, maisha ni ya thamani.”

Ameeleza kuwa licha ya kuwepo kwa kutoelewana kati yake na baadhi ya wanafamilia wa kifalme, amechagua kusamehe:

“Kumekuwa na kutoelewana kwingi kati yangu na baadhi ya familia yangu... lakini sasa nimewasamehe.”

Mwanamfalme huyo aliongeza kuwa suala la usalama limechangia kwa kiasi kikubwa kusambaratika kwa mawasiliano kati yake na baba yake, Mfalme Charles III:

“Mfalme hatazungumza nami kwa sababu ya mambo haya ya usalama,” alisema. “Lakini sikutaka kupigana tena, na kweli sijui baba yangu ana muda gani.”

Harry, ambaye tangu mwaka 2020 anaishi Marekani na mkewe Meghan Markle pamoja na watoto wao wawili, alisema uamuzi wa mahakama wa kumkatalia ulinzi wa daraja la juu akiwa Uingereza umeongeza wasiwasi juu ya kurejea nchini humo:

“Sioni ulimwengu ambao ningemrudisha mke wangu na watoto wangu Uingereza kwa wakati huu,” alisema baada ya hukumu hiyo ya Ijumaa.

Kwa upande wa Ikulu ya Buckingham, ilisema:

“Maswala haya yote yamechunguzwa mara kwa mara na kwa uangalifu na mahakama, na hitimisho sawa katika kila utaratibu.”


Chanzo cha Mvutano Kati ya Harry na Familia ya Kifalme



Tofauti kati ya Mwanamfalme Harry na familia yake ya kifalme zilianza kuonekana wazi mwaka 2020, alipoamua kwa kushirikiana na mkewe kujiondoa katika majukumu rasmi ya kifalme, hatua iliyojulikana kama “Megxit.” Uamuzi huo uliwashtua Wabritania wengi na kuweka uhusiano wake na baba yake, Mfalme Charles, katika hali ya sintofahamu.



Baada ya kujiondoa, Harry na Meghan walihamia Marekani na kuanza kutoa mahojiano ya wazi kuhusu maisha yao ya kifalme. Katika mahojiano yao maarufu na Oprah Winfrey mwaka 2021, walifichua madai ya ubaguzi wa rangi dhidi ya mtoto wao wa kwanza, Archie, na ukosefu wa msaada wa kisaikolojia kutoka ndani ya taasisi ya kifalme. Kauli hizi zilionekana kama kushambulia familia ya kifalme hadharani.

Kwa Harry binafsi, alieleza kuwa alihisi kukosa ulinzi wa baba yake, siyo tu katika usalama wa kimwili bali pia wa kihisia. 


Tangu wakati huo, mawasiliano kati yake na Mfalme Charles yameripotiwa kuwa hafifu au kukatika kabisa.

Mzozo huo ulizidishwa zaidi na Harry kuwasilisha kesi dhidi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza akitaka apewe kiwango cha juu cha ulinzi hata akiwa amejiondoa kwenye majukumu ya kifalme. 


Mahakama ilitupilia mbali madai yake, ikisema hana haki ya kupewa ulinzi huo kwa kutumia fedha za umma.

Licha ya yote hayo, matamshi ya hivi karibuni kutoka kwa Harry yanaonesha tamaa mpya ya kusuluhisha tofauti na kuijenga upya familia iliyosambaratika:

“Sikutaka kupigana tena... maisha ni mafupi, na familia ni muhimu.”

0 Comments:

Post a Comment