Tuesday, May 27, 2025

Msajili Aisitishia CHADEMA Ruzuku, Atishia Kukisitishia Usajili Endapo Wataendelea Kukaidi Maagizo

 

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imetangaza kuisitishia ruzuku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ikieleza kuwa chama hicho kwa sasa hakina uongozi halali wa kusimamia mapato, matumizi na marejesho ya fedha za umma  kwa mujibu wa sheria.



Hatua hiyo imekuja baada ya CHADEMA kuendelea kukaidi maagizo ya Msajili. Jaji Francis Mutungi kuhusu kutotambuliwa kwa Sekretarieti ya chama hicho iliyo chini ya Katibu Mkuu John Mnyika, iliyoteuliwa Januari 22 mwaka huu katika Baraza Kuu lililoongozwa na Mwenyekiti mpya wa chama hicho, Tundu Lissu.

“Kutokana na ombwe la uongozi wa chama hicho, Msajili wa Vyama vya Siasa ameamua kusitisha kuwapa ruzuku chama hicho hadi kitakapotekeleza maelekezo kwa sababu chama hicho hakina viongozi wanaoweza kusimamia mapato na matumizi na marejesho ya fedha hizo za umma,” ilieleza taarifa ya Msajili iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo.

Ofisi hiyo imesisitiza kuwa haitambui Sekretarieti ya sasa ya CHADEMA kwa madai kuwa akidi ya kikao cha Baraza Kuu kilichowateua haikutimia, hivyo uteuzi huo ni batili kikatiba na kikanuni.


Katika orodha ya waliotajwa kutotambuliwa na Msajili ni pamoja na John Mnyika, Amani Golugwa, Ali Ibrahimu Juma, Godbless Lema, Dk. Rugemeleza Nshala, Rose Mayemba, Salima Kasanzu na Hafidhi Ali Saleh.

“Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inawasihi wananchi, wadau, mamlaka na taasisi zote za serikali na binafsi, kutowapa ushirikiano na huduma wanachama walioorodheshwa hapo juu, endapo watahitaji kuzipata kama viongozi wa CHADEMA,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo, ikitaja sheria mbalimbali zinazoipa nguvu Ofisi hiyo kuchukua hatua hizo.

Msajili pia amesema kuwa amesikitishwa na msimamo wa CHADEMA wa kutozingatia maagizo ya kisheria, hususan kauli iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti Bara wa CHADEMA, aliyesema kuwa maamuzi ya Msajili kuhusu malalamiko yaliyowasilishwa na mwanachama Lembrus Mchome ni batili.

“Napenda kuwafahamisha Watanzania kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa amesikitishwa na msimamo huo wa CHADEMA. Wanapaswa kufanya uamuzi wa busara wa kuitisha kikao halali cha Baraza Kuu la Taifa la chama chao na kujaza nafasi zilizowazi, badala ya kubishana na sheria, kwani sheria ni msumeno,” imesisitiza Ofisi hiyo.

Kuhusu tuhuma za kuwa upande wa Mchome, Msajili amekanusha na kusema kuwa alichowasilisha mwanachama huyo siyo rufaa, bali ni malalamiko ya kawaida kama wanavyofanya wanachama wa vyama vingine. Pia ofisi hiyo imesema ilitoa ufafanuzi wa kina juu ya mamlaka yake kushughulikia masuala yanayohusu ukiukaji wa katiba na kanuni za chama.

Msajili ameonya kuwa iwapo CHADEMA itaendelea kukaidi, ataomba mamlaka husika zichukue hatua za kijinai dhidi ya wale wanaojitambulisha kama viongozi kinyume cha sheria.

Aidha, ameonya kuwa yuko tayari kusimamisha usajili wa CHADEMA iwapo chama hicho kitaendelea kutotii maelekezo yake na kuwatambua viongozi ambao ofisi yake haiwatambui kisheria.

Hali hii inaibua mgogoro wa wazi kati ya Msajili wa Vyama na CHADEMA, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipinga kile wanachokiita ni kuingiliwa kwa uhuru wa ndani wa chama na mamlaka za serikali.

Chanzo: Taarifa rasmi ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mei 2025.


No comments:

Post a Comment