Mbunge wa Eneo Bunge la Kasipul, Charles Ong’ondo Were, ameaga dunia kwa njia ya kusikitisha baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana waliokuwa wamepanda pikipiki katika Barabara ya Ngong jijini Nairobi, Jumatano, Aprili 30.
Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula amethibitisha kifo cha mbunge huyo, akisema: “Ni kwa huzuni kubwa ninapopokea taarifa za kuangamia kwa mmoja wa wawakilishi wetu wa kitaifa kwa njia ya kikatili. Tunalaani vikali kitendo hiki cha kinyama.”
Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha Citizen, tukio hilo lilitokea karibu na Hifadhi ya Maiti ya jiji la Nairobi, ambapo mbunge huyo alipigwa risasi na watu wawili waliokuwa wakimfuatilia kwa pikipiki.
Charles Ong’ondo Were alikuwa mwanachama wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Raila Odinga. Taarifa za kifo chake zilisambazwa mapema na mjumbe wa wadi ya Kileleshwa, Robert Alai, kupitia mitandao ya kijamii. Alai aliandika: “Tumehangaika mno kumkinga Ong’ondo Were. Aliwahi kunieleza kuhusu vitisho dhidi ya maisha yake. Sasa tumempoteza.”
Kwa mujibu wa vyanzo vya karibu na marehemu, uchunguzi wa awali unaonesha kwamba alifariki dunia papo hapo kutokana na majeraha ya risasi aliyoyapata katika eneo la tukio. Uchunguzi wa kina unaendelea kufanywa na idara ya upelelezi ya DCI.
Kabla ya kifo chake, Ong’ondo Were alikuwa ametoa malalamiko kuhusu vitisho dhidi ya maisha yake. Katika mahojiano na wanahabari miezi miwili iliyopita, alisema: “Maisha yangu yako hatarini. Kuna watu wanaoleta vurugu kutoka nje ya Kasipul wakilenga kuvuruga amani katika mikutano yangu.”
Alisisitiza kuwa vurugu hizo zimekuwa zikiandamana na mashambulizi ya wazi, ikiwa ni pamoja na kuvurugwa kwa ibada ya mazishi katika wadi ya Nyatindo East Kamagak wiki moja kabla ya kuuawa kwake. Pia alieleza tukio jingine katika eneo la God Nyango ambapo barabara ilifungwa ghafla alipokuwa akielekea kwenye mazishi.
“Mmoja wa wahalifu alinieleza wazi kuwa sitazungumza kwenye mazishi, hata kabla ya maombi kuanza,” alisema Were kwa masikitiko.
Raila Odinga, kiongozi wa ODM, alielezea huzuni yake kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, akisema: “Tumepoteza sauti ya haki na maendeleo. Ong’ondo alikuwa mtetezi wa wanyonge.”
Wakenya wengi wameendelea kueleza masikitiko yao mitandaoni huku wakitaka uchunguzi wa haraka na haki kutendeka kwa familia ya marehemu. Serikali imetoa ahadi ya kuwakamata waliotekeleza mauaji hayo.

No comments:
Post a Comment