Monday, May 26, 2025

Kabila Aibua Mzuka wa Kisiasa: Atangaza Kutembelea Goma, Aitaja Serikali ya Kongo kuwa ya Kidikteta



Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila, ameibuka tena kwenye majukwaa ya kisiasa kwa matamshi mazito dhidi ya serikali ya sasa inayoongozwa na Felix Tshisekedi, akiituhumu kwa kuendesha nchi kidikteta na kwa kutumia taasisi za dola kuwakandamiza wapinzani.




Kupitia hotuba iliyorushwa moja kwa moja katika mitandao ya kijamii, Kabila alieleza kuwa anapanga kutembelea mji wa Goma, ambao kwa sasa unadhibitiwa na waasi wa kundi la M23, kundi ambalo linatajwa kuwa linaungwa mkono na serikali ya Rwanda.

Akizungumzia hatua ya Bunge la DRC kumuondolea kinga ya rais mstaafu, Kabila alisema:

“Siku chache zilizopita, kufuatia uvumi kutoka mitaani au mitandaoni kuhusu madai ya kuwepo kwangu Goma, ambako nitaenda katika siku zijazo kama ilivyotangazwa, utawala mjini Kinshasa ulichukua maamuzi ya kiholela ya kizembe bila kufikiria, na hii inaonesha kupungua kwa demokrasia nchini humo.”

Hatua hiyo ya bunge inaaminika kufungua njia ya yeye kufikishwa mahakamani kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo uhaini, uhalifu wa kivita, na ushiriki katika harakati za uasi – tuhuma ambazo Kabila amezikana vikali.

Katika hotuba hiyo, Kabila mwenye umri wa miaka 53, alimtuhumu moja kwa moja Rais Felix Tshisekedi, kwa kulihujumu jina lake na kuendesha nchi kwa mtindo wa kidikteta.

“Utawala wa sasa umejaa udikteta. Demokrasia lazima irejeshwe Kongo. Tunahitaji hali bora ya uchumi na utawala unaowajali watu,” alisema Kabila kwa msisitizo.

Kabila, ambaye aliongoza DRC kuanzia mwaka 2001 hadi 2019, amesema hatua ya serikali ni njama za kisiasa za kumkomoa kwa kisingizio cha ushirikiano na waasi.

“Serikali imeamua kuniondolea kinga kutokana na uvumi tu, bila ushahidi wowote, na hii ni dalili ya uongozi unaoogopa kivuli chake,” alisema.

Rais wa sasa, Felix Tshisekedi, awali alidai kuwa Kabila ana uhusiano wa karibu na kundi la waasi la M23, ambalo linashutumiwa kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu mashariki mwa nchi hiyo. Serikali ya Kongo imekuwa ikipambana na kundi hilo kwa miaka kadhaa sasa.

Kabila, hata hivyo, amesisitiza kuwa ziara yake ya Goma siyo ya kichokozi, bali ni ya kawaida kama raia na kama kiongozi mstaafu anayetaka “kuona hali halisi ya wananchi wake”.

“Siogopi. Nitakwenda Goma. Niko tayari kwa lolote lakini sitanyamaza mbele ya dhuluma na kuvunjwa kwa misingi ya kidemokrasia,” alieleza.

Hii ni mara ya kwanza kwa Kabila kuzungumza hadharani kwa mtindo wa wazi na wa kupambana tangu aondoke madarakani mwaka 2019. Kauli zake zimepokewa kwa hisia tofauti nchini Kongo, ambapo baadhi wanaziona kama dalili za kujiandaa kurudi tena katika siasa za mstari wa mbele.

[Chanzo: https://p.dw.com/p/4u

No comments:

Post a Comment