CHADEMA Wamgomea Msajili wa Vyama vya Siasa, Wasisitiza: “No Reforms, No Election”

 


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa tamko kali likimkosoa Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuingilia maamuzi ya ndani ya chama na kuvuka mipaka ya kisheria. 



Tamko hilo limetolewa baada ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichofanyika kwa siku mbili mfululizo, tarehe 23 na 24 Mei 2025.



Akizungumza mara baada ya kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, alisema:

“Kamati Kuu imejiridhisha kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa amekiuka sheria kwa kuingilia masuala ya ndani ya CHADEMA. Maamuzi yake ni batili, hayana msingi wowote wa kisheria na yanaonyesha nia ya makusudi ya kukihujumu chama.”

Heche alifafanua kuwa kikao cha Baraza Kuu cha tarehe 22 Januari 2025 kilikuwa cha kuthibitisha uteuzi wa viongozi, si cha uchaguzi kama inavyodaiwa.

“Msajili hana mamlaka ya kupokea wala kuamua malalamiko ya mwanachama wa chama kingine. Tunamtaka ajisahihishe mara moja na aache uonevu dhidi ya CHADEMA,” aliongeza.

“No Reforms, No Election” si Kauli Tu, Ni Msimamo Rasmi



Katika maazimio ya kikao hicho, CHADEMA imesisitiza kuwa haitashiriki uchaguzi wowote bila mabadiliko ya msingi ya mfumo wa uchaguzi. Kupitia kampeni ya “No Reforms, No Election”, chama kimepanga kuendelea na ziara katika kanda mbalimbali nchini. Ziara ya kwanza itaanza katika Kanda ya Kaskazini tarehe 28 Mei hadi 1 Juni 2025.

“Mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi ni hitaji la Watanzania. CHADEMA tutasimamia msimamo huu kwa nguvu zote. Hatutashiriki tena kwenye uchaguzi wa kinyume cha haki,” alisema Heche.

CHADEMA Yalaani Vitendo vya Utekaji na Unyanyasaji

Katika kikao hicho, Kamati Kuu ilieleza kusikitishwa kwake na matukio ya ukatili dhidi ya wanachama na viongozi wake. Tukio la kutekwa kwa mwanachama wao Mdude Nyagali tarehe 2 Mei 2025 limeelezwa kuwa ni mfano wa matukio ya kiharamia yanayofanywa dhidi ya wapinzani.

“Tumefika mwisho wa kuvumilia. Utekaji, vipigo, na vitisho dhidi ya wanachama wetu vimepamba moto. Huu ni ukandamizaji wa wazi wa haki za binadamu unaoratibiwa na vyombo vya dola,” alisema Heche.

Majeruhi wa matukio hayo ni zaidi ya kumi na tano, wengi wao wakielezwa kuvunjwa viungo na kupigwa vibaya, akiwemo Mkurugenzi wa Mafunzo John Pambalu na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Ally Ibrahim Juma.

Walio Kamatwa Kutoka Nje Nao Waguswa

CHADEMA pia imelaani kukamatwa kwa wanaharakati wa kimataifa – Boniface Mwangi (Kenya) na Agather Atuhaire (Uganda), waliotekwa na kusafirishwa kwa nguvu kutoka Tanzania.

“Tulifuatilia suala hili polisi. Boniface alisafirishwa kwa gari, Agather kwa ndege akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi. Hili ni jambo la aibu kwa taifa letu,” alisema Heche.

Kauli ya Rais Yakosolewa

Katika tamko hilo, CHADEMA pia imekosoa kauli ya Rais aliyoitoa tarehe 19 Mei 2025 wakati wa uzinduzi wa sera ya mambo ya nje, wakisema kuwa imekosa hekima ya kidiplomasia na inaweza kuhatarisha mshikamano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Kauli ile inapaswa kurekebishwa. Haiakisi maslahi ya taifa wala majirani zetu wa kikanda,” aliongeza Heche.


0 Comments:

Post a Comment