Monday, May 26, 2025

“CCM Haijali Kususiwa” – Othman Masoud Aweka Wazi Sababu za ACT Wazalendo Kushiriki Uchaguzi 2025





“CCM haitaki kususiwa uchaguzi — wanatumia ususiaji kama fursa ya kujipatia ushindi wa mezani,” amesema Mwenyekiti wa ACT Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, katika kikao maalum kilichofanyika Mei 25, 2025 mjini Bariadi, Simiyu.


Amesema uzoefu wa kihistoria umeonesha kuwa kususia uchaguzi hakujawahi kuizuia CCM kuendelea kujipatia ushindi wa mashaka, bali huipa mwanya wa kutawala bila changamoto.

“Sisi tunaamini njia sahihi ni kupambana nao kwa kuhamasisha wananchi wajitokeze na kutumia nguvu yao ya kura,” alisisitiza.


Kauli hiyo ilikuwa majibu kwa hoja zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama rafiki vya upinzani waliotaka ACT Wazalendo kuungana na msimamo wa kutoshiriki uchaguzi bila marekebisho ya msingi ya sheria za uchaguzi na tume huru.

Ntemi Jackson Lubelele, Mwekahazina wa CHADEMA Wilaya ya Bariadi, alihoji:
“Kwa nini ACT Wazalendo haijaungana nasi katika msimamo wa No Reform No Election?”
Alisisitiza kuwa kushiriki uchaguzi bila mabadiliko ya msingi ni kuh legitisha mfumo dhalimu.

Ngulima Sita, Katibu wa CHAUMMA Mkoa wa Mara, naye aliuliza:
“ACT Wazalendo inajipangaje kukabiliana na hujuma za waziwazi kama zilizojitokeza kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024?”

Katika majibu yake, Othman Masoud alisisitiza kuwa chama hicho hakitegemei mfumo pekee kubadilisha hali ya siasa, bali kinawategemea wananchi.
“Mtaji wetu mkubwa ni wananchi. Sio tu kwamba tunawatumia kama wapiga kura, bali tunawaandaa kuwa walinzi wa haki yao ya kuchagua,” alisema.
“Hatutakubali tena uchaguzi unaoendeshwa kwa mazoea ya hila na vitisho.”

Alifafanua kuwa ACT Wazalendo inaingia kwenye uchaguzi kwa maamuzi ya kimkakati, huku ikijifunza kutokana na historia ya hujuma tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
“Tumejifunza. CCM si chama cha kutumikia watu tena — ni biashara ya utajiri wa viongozi. Hatuwezi kuikimbia, lazima tupambane tukiwatumia wananchi kama ngao na silaha yetu,” alihitimisha.

Kikao hicho kililenga kujenga uelewa wa pamoja miongoni mwa vyama vya upinzani kuhusu mustakabali wa siasa za upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.


No comments:

Post a Comment