Balile: Waandishi Zingatieni Taratibu Kuripoti Kesi ya Lissu



 Waandishi wa habari watakaoripoti kesi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wametakiwa kuwa na kitambulisho halali cha kazi na kuvaa jaketi maalum linalowatambulisha kama waandishi wa habari, ili kuruhusiwa kuingia mahakamani kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo.



Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, ametoa wito huo leo jijini Dar es Salaam, akisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu rasmi na kufanya kazi kwa weledi, hasa katika kuripoti kesi nyeti zinazohusisha masuala ya kisiasa na usalama wa taifa.

“Mwandishi hapaswi kuzuiwa kufanya kazi yake ya kuujulisha umma, hasa katika kesi nyeti kama ya Tundu Lissu, kwani jamii nayo ina haki ya kujua kinachoendelea,” amesema Balile.

Balile amesema tayari TEF imekutana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, ambapo walikubaliana kuwa waandishi waruhusiwe kuingia mahakamani kusikiliza kesi hiyo, lakini kwa masharti ya kuzingatia taratibu zinazojulikana.

Ameeleza kuwa uandishi wa habari unapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia sheria, maadili ya taaluma, pamoja na kuhakikisha usalama wa waandishi na wale wanaohusika katika taarifa wanazoripoti.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam, Bakari Kimwanga, amewakumbusha waandishi kuzingatia usalama wao binafsi wanapotekeleza majukumu yao, hasa katika mazingira yenye hisia kali kama maeneo ya mahakama.

“Swala la usalama linaanza na wewe kabla ya mtu yeyote. Unapoanza kutekeleza majukumu yako, unapaswa kufuata taratibu zote ili kupunguza changamoto zinazoweza kukukuta ukiwa kazini,” amesema Kimwanga.

Kesi ya Tundu Lissu imekuwa gumzo nchini kutokana na uzito wa mashtaka ya uhaini na uchochezi yanayomkabili, huku ikivuta hisia za wananchi na vyombo vya habari. Waandishi wametakiwa kuwa makini, wakitoa taarifa sahihi, za kina na zenye kuzingatia maadili ya taaluma ya habari.

0 Comments:

Post a Comment