Sunday, May 25, 2025

Arusha Kuwa Mwenyeji wa Mkutano Mkubwa wa 33 wa Wakuu wa Majeshi wa SADC



Mkoa wa Arusha umechaguliwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 33 wa mwaka wa Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 26 hadi 31 Mei 2025.

Mkutano huo mkubwa utawakutanisha viongozi wa kijeshi kutoka zaidi ya nchi 15 wanachama wa SADC, na ni miongoni mwa mikutano ya juu inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na usalama katika ukanda huo.



Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Mkoa wa Arusha, 26 Mei 2025, Mkuu wa Mkoa wa huu , Paul Makonda, alisema kuwa uteuzi wa Arusha kuwa mwenyeji wa mkutano huo ni heshima kubwa kwa mkoa huo na Taifa kwa ujumla.

“Arusha imeendelea kuwa kinara wa mikutano ya kitaifa na kimataifa. Pia ni kitovu cha shughuli za utalii ambazo zimekuwa zikichochea uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla. Mkutano huu ni fursa nyingine muhimu ya kuonyesha uwezo wetu katika utoaji wa huduma bora kwa wageni wa kimataifa,” alisema Makonda.

Makonda alieleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa mstari wa mbele kudumisha amani na utulivu nchini — hali inayowafanya wawekezaji na watalii kuvutiwa kuja Tanzania, hususan Arusha.

“Mazingira ya utulivu ndiyo msingi wa maendeleo ya kweli. Bila amani, mikutano kama hii isingekuwa rahisi kufanyika hapa nchini. Hii ni fursa kubwa ya kuutangaza mkoa wetu kimataifa,” aliongeza Makonda.

Kwa upande wake, Jenerali Jacob Mkunda, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Tanzania (CDF), ambaye ni mwenyekiti wa mkutano huo, ataongoza majadiliano yatakayojikita katika kuimarisha ushirikiano wa usalama na kukabiliana na changamoto za kijeshi za ukanda wa SADC.

Wakati wa mkutano huo, wajumbe watapata pia fursa ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo mkoani Arusha, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuunga mkono sekta ya utalii na kuongeza mapato kwa wakazi wa eneo hilo.

Makonda alitoa wito kwa wadau wa huduma mbalimbali kuhakikisha wanatoa huduma bora, ukarimu na kuwahudumia wageni kwa weledi ili kuchochea fursa za kiuchumi zitakazotokana na mkutano huo.

“Watoa huduma kwenye hoteli, usafirishaji, biashara na maeneo yote wahakikishe wanatoa huduma bora. Wageni hawa wanapokuja, wanatoa fursa nyingi kwa biashara zetu na kwa jamii kwa ujumla,” alisema.

Katika hatua nyingine, Makonda aliwataka wananchi wa Arusha kutokuwa na hofu juu ya uwepo wa magari ya kijeshi na wanajeshi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, akifafanua kuwa hayo ni maandalizi ya kawaida kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa mkutano huo muhimu.

“Wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida. Huu ni mkutano mkubwa, maandalizi yanahusisha ulinzi wa kutosha. Tushirikiane na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha amani inaendelea kutawala,” alisema.

No comments:

Post a Comment