Dar es Salaam – Wafanyabiashara 50 waliokuwa wakifanya biashara katika jengo lililoporomoka eneo la Kariakoo mnamo Novemba 16, 2024, wamefungua kesi katika Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi wakidai fidia ya Shilingi bilioni 40 kutoka kwa wamiliki wa jengo hilo kutokana na hasara ya biashara na uwekezaji waliopata.
Katika hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani na wakili wao, Peter Madeleka, walalamikaji wakiongozwa na Kanali Naftal Swai wanadai kuwa uzembe wa wadaiwa katika kufanya ujenzi wa chini kwa chini bila idhini na kinyume na masharti ya mkataba wa upangaji, ndio ulisababisha jengo hilo kuporomoka.
"Wateja wangu walipata hasara kubwa kutokana na kuporomoka kwa jengo hilo, ambapo biashara na uwekezaji wao wa zaidi ya Shilingi bilioni 40 uliharibiwa," alisema Wakili Peter Madeleka. "Wamiliki wa jengo walikiuka makubaliano ya upangaji kwa kufanya ujenzi usioidhinishwa, uliopelekea hatari kwa wapangaji."
Wadaiwa katika kesi hiyo ni pamoja na Zenabu Ismail, anayesemekana kuwa mwakilishi wa kisheria wa marehemu Abdallah Salim; Ashour Ashour, mwakilishi wa marehemu Awadhi Ashur Abeid; na Leondela Mdete. Walalamikaji wanataka mahakama itamke kuwa wadaiwa hao walikiuka mkataba wa upangaji kwa kufanya ujenzi wa kizembe.
Katika hati hiyo ya madai, imeelezwa kuwa kati ya Januari 2023 hadi Desemba 31, 2024, walalamikaji waliingia mikataba ya upangaji wa mdomo na maandishi na wadaiwa kuhusu jengo hilo lililopo Kiwanja namba 12, Kitaru 7, Kariakoo, Manispaa ya Ilala.
"Ujenzi huo wa chini kwa chini ulifanyika bila idhini ya wapangaji na kinyume na masharti ya mkataba. Hatua hiyo ilisababisha jengo kuporomoka, na hivyo kuharibu biashara zetu za rejareja na jumla," wamesema walalamikaji katika hati yao.
Mbali na fidia hiyo ya Sh bilioni 40, walalamikaji pia wanaomba mahakama itoe hukumu ya kuwataka wadaiwa kulipa gharama za kesi hiyo.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Mohamed Gwae na ilitajwa kwa mara ya kwanza Aprili 29, 2025 mbele ya Naibu Msajili Rose Kangwa.

No comments:
Post a Comment