Uchaguzi Mkuu wa 2025: Hakuna Atakayezuia na Haki ya Kichagua na Kuchaguliwa Itaheshimiwa

 


Uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 umeendelea kuwa kipengele cha mjadala wa kisiasa nchini, huku viongozi wakitoa kauli mbalimbali kuhusu mchakato na ushiriki wa vyama vya siasa, hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). 


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amesisitiza kuwa uchaguzi huo utaenda kama ilivyoelekezwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hakuna mamlaka yoyote itakayoweza kuzuia mchakato huo.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu Maalum wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) uliofanyika leo Ijumaa, Aprili 4, 2025 mjini Songea, Dkt. Nchimbi alisisitiza kuwa uchaguzi wa Rais, wabunge, na madiwani mwaka 2025 utaendelea kama ilivyo agizwa na sheria.

"Nchi yetu ina utaratibu wa kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano. Hakuna raia yeyote, hata Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu mwenye mamlaka ya kusema uchaguzi hautafanyika," alisisitiza Dkt. Nchimbi.

Kauli hii ya Katibu Mkuu wa CCM inakuja baada ya mjadala mkubwa unaoendelea kuhusu ushiriki wa vyama vya siasa katika uchaguzi huo, ambapo baadhi ya viongozi na wananchi wamekuwa wakishinikiza CHADEMA kushiriki uchaguzi, licha ya msimamo wa chama hicho dhidi ya kushiriki bila mabadiliko ya kisheria.

Dkt. Nchimbi alieleza kuwa, ingawa kila raia ana haki ya kugombea, hakuna chama kinachoweza kulazimishwa kushiriki uchaguzi, kwani ni haki yao ya msingi. "Ni haki yao kususia na uchaguzi huu sio wa mwisho, nataka niwape salamu zao CHADEMA...Kuna uchaguzi mwingine mwaka 2030, 2035, 2040, 2045 na 2050. Wasipoupata huu, wataupata ule mwingine," alisema.

Pia, Dkt. Nchimbi alikemea tabia ya kuwakejeli au kuwalazimisha wapinzani kushiriki uchaguzi, akisisitiza kuwa "Kukaa kuwasema sema CHADEMA ni kinyume cha sheria na katiba. Mtu yeyote asiwalazimishe CHADEMA kuingia kwenye uchaguzi."

Katika hatua nyingine, Dkt. Nchimbi aliendelea kusema kuwa Katiba inaruhusu uchaguzi kufanyika hata kwa chama kimoja pekee, na kwamba raia wana haki ya kuchagua hata kama hawataki kugombea. "Ukikosa haki ya kuchaguliwa, unapata haki ya kuchagua. Katika haki mbili, unapata moja na unakuwa umejitendea haki kama raia wa Tanzania," aliongeza.

Kauli za Dkt. Nchimbi zimekuja baada ya msimamo wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ambaye alisisitiza kuwa chama hicho hakiwezi kushiriki uchaguzi bila mabadiliko muhimu ya kisheria. Katika mkutano na wanachama wa CHADEMA uliofanyika Dar es Salaam, Lissu alisisitiza kwamba "Bila mabadiliko hakuna uchaguzi, na katika hilo hatanii." Lissu alifafanua zaidi kuwa kama wanachama wa CHADEMA hawako tayari kufuata msimamo huo, milango iko wazi kwao, kwani hakuna atakayeshikiwa bunduki kulazimishwa kushiriki. "No Reform No Election," alisisitiza Lissu, akiweka bayana msimamo wa chama chake kuhusu mabadiliko ya kisheria kabla ya uchaguzi.

Katika hali hii ya kisiasa, Dkt. Nchimbi alisisitiza kuwa kila chama cha siasa kina haki ya kufanya maamuzi yake, na kama CHADEMA watakataa kushiriki uchaguzi huu, wataheshimu haki yao, na kwamba uchaguzi huo utaendelea kama ilivyoelekezwa na Katiba.

"Kugombea na kutogombea vyote ni sawa, ni haki yao. Hata hivyo kama watagomea wasisahau kura zao au sio… ndio jadi yetu kwani ukikosa haki ya kuchaguliwa usipoteze haki ya kuchagua," alisema Dkt. Nchimbi.

Hii ni sehemu ya mjadala wa kisiasa unaoendelea nchini Tanzania, ambapo masuala ya mabadiliko ya kisheria, haki za vyama vya siasa na ushiriki katika uchaguzi ni miongoni mwa mada zinazozungumziwa sana. Hata hivyo, suala kuu linabakia kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 utaendelea, na kila raia ana haki ya kuchagua au kuchaguliwa kulingana na matakwa ya Katiba.

0 Comments:

Post a Comment