Klabu ya Simba Sports Club imeandika ukurasa mpya katika historia ya soka barani Afrika baada ya kufuzu kwa fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup), kwa kuiondosha Stellenbosch FC ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 1-0.
Katika mchezo wa marudiano uliopigwa kwenye Uwanja wa Moses Mabhida jijini Durban, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana (0-0). Matokeo hayo yaliihakikishia Simba tiketi ya fainali kwa faida ya ushindi wa bao 1-0 walioupata katika mchezo wa kwanza uliochezwa katika Uwanja wa Amaan, Visiwani Zanzibar.
Hii ni mara ya pili kwa Klabu ya Simba kufika hatua ya fainali katika michuano ya CAF, mara ya kwanza ikiwa ni mwaka 1993. Safari hii, Wekundu wa Msimbazi wanasubiri mshindi kati ya CS Constantine ya Algeria na RS Berkane ya Morocco.
Fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho CAF imepangwa kuchezwa Mei 17, 2025, huku mchezo wa marudiano ukichezwa Mei 25, 2025.
Kombe la Shirikisho Afrika lilianzishwa mwaka 2004 baada ya kuunganishwa kwa mashindano ya African Cup Winners' Cup (iliyodumu kuanzia mwaka 1975) na CAF Cup (iliyodumu kuanzia 1992).
RAIS SAMIA AIPONGEZA SIMBA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Klabu ya Simba kwa ushindi huo mkubwa na mafanikio ya kufuzu kwa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kupitia salamu zake, Rais Samia alisema:
"Pongezi za dhati kwa Klabu ya Simba kwa ushindi katika mchezo wa Mashindano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF Confederation Cup), na kuandika historia ya kufika fainali ya mashindano haya. Mmeipa nchi yetu heshima kubwa. Nawatakia kila kheri. Mnayo hamasa yangu wakati wote."
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Simba SC, alieleza furaha yake kwa mafanikio hayo akisema:
"Tumefanya kazi kubwa kama timu. Kila mchezaji alijitoa, na sasa tumefikia hatua ya kihistoria. Lengo letu ni kuhakikisha tunaleta kombe nyumbani."
Nahodha wa timu hiyo naye aliongeza:
"Tumeandika historia, lakini safari haijaisha. Tuna deni kwa mashabiki wetu, na tunataka kuhitimisha kazi tuliyoianza."
Mashabiki wa soka Tanzania sasa wana kila sababu ya kujivunia mafanikio ya Simba SC, wakisubiri kwa hamu fainali ya kihistoria ambayo huenda ikaleta kombe la kwanza la CAF nchini Tanzania.
▼

No comments:
Post a Comment