Wizara hii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeweka mifumo ya kisheria inayomlinda kila mmoja dhidi ya ukatili wa aina yoyote ile.
Tumeandaa madawati ya jinsia kwenye taasisi zote za umma ikiwemo shuleni, vyuoni pamoja na kwenye taasisi zinazotoa huduma za kiulinzi kama Jeshi la Polisi na Magereza.
Kauli hiyo imetolewa leo, Alhamisi Aprili 24, 2025 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Stella Simon Fiyao aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kuandaa vitengo maalum katika shule, vyuo, jamii na ofisi kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na ukatili.
Katika majibu yake, Majaliwa alisema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mikakati madhubuti ya kupambana na ukatili, ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu kwa jamii na ushirikiano na taasisi mbalimbali zinazopinga ukatili.
Alieleza kuwa Serikali imechukua hatua za makusudi kwa kuunda wizara maalum inayoshughulikia masuala ya kijamii, ambayo ina jukumu la kuhakikisha kuwa haki, usalama na utu vinadumishwa katika jamii.
“Katika kuhakikisha nchi inakuwa salama dhidi ya ukatili kwenye jamii, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliunda wizara maalum inayosimamia masuala ya kijamii pamoja na kuhakikisha inakabiliana na ukatili kwenye jamii,” alisema.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia wizara hiyo imeanzisha madawati ya jinsia katika taasisi zote za umma, ili kutoa nafasi kwa waathirika wa ukatili kupata msaada wa haraka na ushauri wa kitaalamu.
Majaliwa alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya ukatili ni jukumu la kila Mtanzania, akihimiza ushiriki wa kila mmoja katika kulinda na kutetea haki za binadamu.
“Matukio haya ambayo yanajitokeza katika jamii, yanaondoa haki ya msingi ya kibinadamu pale mtu anapotendewa ukatili dhidi yake. Hivyo kila mmoja awe mlinzi wa matendo haya popote pale,” alisisitiza.

No comments:
Post a Comment