SERIKALI KUTUMIA MILIONI 17 KUWEKA NISHATI SAFI LONGIDO SAMIA GIRLS


 



Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko, amesema Serikali itagharamia gharama ya shilingi milioni 17 kwa ajili ya kuweka miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika Shule ya Sekondari ya Longido Samia Girls iliyopo wilayani Longido, mkoani Arusha.



Dkt. Biteko alitoa kauli hiyo leo Aprili 24, 2025, wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani humo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.



“Serikali inataka kuhakikisha shule hii mpya inatumia nishati safi na salama kwa mazingira, na ndio maana tumeamua kugharamia miundombinu hiyo kwa fedha za serikali,” alisema Dkt. Biteko.



Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko aliagiza viongozi wa mkoa kuhakikisha vifaa vya maabara vinakamilika na kuwekwa katika maabara zote nne za sayansi zilizopo shuleni hapo. 



“Wanafunzi lazima wajifunze kwa vitendo, si kutegemea nadharia pekee. Serikali haitaridhika hadi kila mwanafunzi apate mazingira bora ya kujifunza,” aliongeza.



Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita imeleta mageuzi makubwa katika elimu na kuahidi kutekeleza kwa wakati maagizo yote yaliyotolewa.



“Tutahakikisha uzio wa shule unajengwa, vifaa vya maabara vinapatikana na kila agizo linatekelezwa. Natoa wito kwa wazazi kuwapeleka watoto wao shule ili wapate elimu bora na kufikia ndoto zao,” alisema Makonda.



Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Longido Samia Girls, Esther Kobelo, alisema shule hiyo ni miongoni mwa shule 26 mpya zilizoanzishwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kukuza elimu ya sayansi kwa wasichana nchini.



“Shule ilifunguliwa Januari 7, 2024, ikiwa na wanafunzi 310 wa kidato cha kwanza na cha tano, wote wakisomea masomo ya sayansi. Tuna walimu 16, kati yao wakiwa wanne ni walimu wa kike na tuna mtaalamu mmoja wa maabara,” alisema Kobelo.



Ujenzi wa shule hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali kuimarisha mazingira ya kujifunzia kwa wasichana na kuongeza usawa katika upatikanaji wa elimu ya sayansi nchini.



0 Comments:

Post a Comment