Rais, Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Mmiliki wa Klabu ya Manchester United ya Uingereza, Sir Jim Ratcliffe, tarehe 11 Aprili, 2025, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, Rais Samia alimkaribisha rasmi Sir Jim kuwekeza nchini Tanzania, hususan katika sekta za michezo na utalii.
Mazungumzo kati ya viongozi hao wawili yalilenga kuangazia fursa za ushirikiano baina ya Tanzania na klabu ya Manchester United, ambayo ina mashabiki mamilioni duniani kote, wakiwemo wengi kutoka barani Afrika.
Akizungumza katika kikao hicho, Sir Jim Ratcliffe alionesha nia ya kuitumia Manchester United kama jukwaa la kuitangaza Tanzania kimataifa, hasa kupitia kampeni za utalii.
"Tunaamini Tanzania ina vivutio vya kipekee vya utalii ambavyo dunia inapaswa kuviona. Kupitia Manchester United, tunaweza kusaidia kuitangaza Tanzania kwa hadhira kubwa zaidi," alisema Sir Jim.
Katika ishara ya heshima na urafiki, Sir Jim alimkabidhi Rais Samia jezi ya Manchester United iliyosainiwa na wachezaji wa timu hiyo. Rais Samia alipokea zawadi hiyo kwa furaha na shukrani, na kutumia fursa hiyo kumualika mwekezaji huyo kuangalia uwezekano wa kuanzisha vituo vya mafunzo ya michezo (Sports Academies) nchini.
“Nakukaribisha uweze kuanzisha vituo vya kukuza vipaji kwa vijana wetu. Tuna vijana wengi wenye vipaji vya michezo, lakini wanakosa fursa. Kupitia ushirikiano huu, tunaweza kuwasaidia kufikia ndoto zao,” alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia alitoa pongezi kwa Sir Jim kupitia Taasisi yake ya Six Rivers, ambayo imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) katika kuhifadhi mazingira na kudhibiti muingiliano wa wanyamapori na binadamu.
"Nashukuru kwa kazi nzuri mnayofanya kupitia Taasisi ya Six Rivers. Ushirikiano wenu na taasisi zetu umesaidia sana kulinda bioanuwai na kuhakikisha uhifadhi endelevu," aliongeza Rais Samia.
Kwa upande wake, Sir Jim alieleza dhamira ya Taasisi yake ya Six Rivers katika kurejesha hadhi ya Hifadhi ya Taifa ya Selous.
“Tunataka kuona Selous ikiwa na idadi kubwa ya wanyama wakubwa kama zamani. Ni dhamira yetu kuhakikisha hifadhi hii inakuwa kivutio kikubwa cha utalii wa kimataifa,” alieleza.
Manchester United imekuwa na historia ya kushirikiana na mataifa mbalimbali barani Afrika kupitia miradi ya kijamii inayotekelezwa na Manchester United Foundation. Hata hivyo, huu ni mwanzo wa aina yake kwa mmiliki wa klabu hiyo kuonesha nia ya kuwekeza moja kwa moja katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Ziara ya Sir Jim Ratcliffe nchini Tanzania inaonekana kuwa hatua muhimu ya kuimarisha diplomasia ya michezo na kufungua milango ya ushirikiano wa kimkakati kati ya sekta ya michezo, utalii na maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
0 Comments:
Post a Comment