Katika Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Arusha, viongozi wa serikali wametoa rai kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence) katika tasnia ya habari, wakisisitiza kuwa teknolojia hiyo itumike kama chombo cha maendeleo badala ya kuwa kikwazo kwa uhuru wa habari.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza katika Hoteli ya Gran Melia leo Aprili 29, 2025, amesema kuwa maendeleo ya teknolojia yameleta changamoto na fursa mpya kwa vyombo vya habari, hivyo ni muhimu kwa wanahabari kutumia Akili Mnemba kwa busara na kwa kuzingatia misingi ya taaluma ya habari.
“Ni ukweli usiopingika kwamba, Akili Mnemba inaweza kuwa msaada mkubwa kwa wanahabari, lakini pia inaweza kuwa chanzo cha changamoto kubwa ikiwa haitatumika kwa busara. Hili linahitaji mjadala wa wazi, sera madhubuti, na ushirikiano wa karibu kati ya sekta zote,” alisema Majaliwa.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuandaa sera maalum ya Akili Mnemba ambayo itatoa mwongozo wa matumizi yake katika sekta ya habari ili kuhakikisha teknolojia hiyo inazingatia misingi ya uhuru wa vyombo vya habari, uwazi na uadilifu wa habari.
“Serikali ya Tanzania inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika maendeleo ya Taifa. Kupitia vyombo vya habari, wananchi wamepata taarifa kuhusu shughuli za Serikali na kuhamasika kushiriki katika maendeleo ya nchi yao,” aliongeza.
Aidha, amewahimiza waandishi wa habari kuendelea kufanya kazi kwa weledi, maadili na uzalendo kwa ajili ya maslahi ya taifa na ustawi wa jamii.
“Vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kulinda amani, mshikamano na kuijenga taswira chanya ya Tanzania kimataifa,” alisema Majaliwa.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi alisema kuwa waandishi wa habari hawapaswi kuruhusu teknolojia kuwavuruga, bali waitumie kwa ufanisi na ubunifu.
“Akili Mnemba isiwafanye waandishi wa habari nchini wakafubaa, bali wahakikishe wanaitumia vizuri katika utekelezaji wa majukumu yao,” alisema Kabudi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa aliwapongeza waandishi wa habari kwa kuendelea kupambania matumaini ya wananchi na kuwa daraja kati ya jamii na serikali.
“Tunawapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya licha ya changamoto, kwani mmekuwa daraja la kuwafikishia wananchi taarifa muhimu za maendeleo,” alisema Msigwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, alitoa wito kwa waandishi wa habari kutumia kalamu zao kujenga jamii na kuhamasisha mshikamano badala ya kuchochea migogoro au kueneza hofu.
“Waandishi wa habari wanaweza kuamua jamii iwe vipi kupitia kazi zao, kama vile mavazi, chakula na mwenendo wa maisha. Kalamu yao ina nguvu kubwa,” alisema Makonda.
Pia alialika wanahabari kushiriki Jukwaa la Kiuchumi litakalofanyika Mei 3, 2025, mkoani Arusha, akisema ni fursa muhimu kwao kupata taarifa sahihi na kuzifikisha kwa wananchi ili kuchochea maendeleo.
Maadhimisho haya yamewakutanisha wanahabari, viongozi wa serikali na wadau wa habari kutoka maeneo mbalimbali nchini, yakiwa ni jukwaa muhimu la kuendeleza mazungumzo kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika maendeleo ya taifa na matumizi sahihi ya teknolojia mpya.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni:
“Uhabarishaji kwenye Dunia Mpya: Mchango wa Akili Mnemba (AI) katika Uhuru wa Vyombo vya Habari.”
No comments:
Post a Comment