Hazina na TANAPA Wapitia Bajeti ya TANAPA Mwaka 2025/2026

 


Ofisi ya Msajili wa Hazina imekutana na Wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kujadili na kupitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026. 



Kikao hicho kimefanyika leo, Aprili 10, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.

Bajeti hiyo imeweka kipaumbele katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuongeza fursa za uwekezaji, kuanzisha mazao mapya ya utalii, kuboresha miundombinu ya utalii, na kuimarisha ulinzi mkakati kwa kutumia teknolojia. 


Vipaumbele vingine ni pamoja na kuendeleza shughuli za uhifadhi na tafiti, kuongeza ajira kwa kuzingatia viwango vya kimataifa (ISO), kudhibiti mimea vamizi pamoja na wanyamapori wakali na waharibifu, kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii zinazozunguka hifadhi, na kutekeleza miradi ya maendeleo.



Kikao hicho kiliongozwa na Peter Maungo, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Mashirika ya Kibiashara ya Umma, ambaye alisisitiza umuhimu wa "kupitisha bajeti yenye tija kwa mustakabali wa uhifadhi wa maliasili za taifa letu."



Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Juma Nassoro Kuji, alieleza kwa kina mwelekeo wa kimkakati wa shirika kwa mwaka wa fedha ujao, akisema kuwa:

"Tumejikita katika kuongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali, kuimarisha mifumo ya usimamizi, pamoja na kukuza ushirikiano kati yetu na wadau mbalimbali wa uhifadhi na utalii."


Kamishna Kuji aliambatana na wataalamu waandamizi kutoka idara mbalimbali za TANAPA, waliotoa michango yao katika kujadili na kuboresha bajeti hiyo kabla ya kupitishwa rasmi.

Bajeti hii mpya inaakisi dhamira ya TANAPA ya kuendeleza uhifadhi endelevu, huku ikichochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa taifa kupitia sekta ya utalii.

0 Comments:

Post a Comment