Thursday, April 24, 2025

DKT. BITEKO AFURAHISHWA UKUSANYAJI MAPATO NAMANGA, AAGIZA UJENZI WA KITUO CHA KUPOZA UMEME LONGIDO

 




Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko, amesema ameridhishwa na ongezeko la ukusanyaji wa mapato katika Kituo cha Huduma za Pamoja cha Namanga, mpakani mwa Tanzania na Kenya, na ameagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuharakisha ujenzi wa kituo cha kupokea, kupoza na kusafirisha umeme wilayani Longido ili kuboresha upatikanaji wa nishati katika eneo hilo.



Dkt. Biteko alitoa maelekezo hayo Aprili 24, 2025, akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Arusha, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.



“Nimefurahishwa sana na namna mnavyohamasisha biashara. Mmekusanya shilingi bilioni 101 kati ya lengo la bilioni 124 huku zikiwa zimebaki miezi kadhaa kabla ya mwaka wa fedha kuisha. Hii ni hatua kubwa,” alisema Dkt. Biteko, akiipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kazi nzuri inayofanywa katika kituo hicho.



Aliwataka watendaji wa kituo hicho kuendelea kuboresha huduma kwa kupunguza muda wa kushughulikia mizigo kutoka saa mbili hadi dakika 30 hadi 40 ili kuharakisha biashara na kuongeza tija kwa wafanyabiashara.



Katika ziara hiyo, Dkt. Biteko alitembelea pia Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Longido Samia, ambapo alieleza kuwa Serikali kupitia Kampuni ya Taifa ya Gesi itasimamia ufungaji wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia shuleni hapo.



“Shule hii ni sehemu ya dira ya Serikali ya kuimarisha matumizi ya nishati safi na salama. Tumejipanga kuhakikisha mfumo wa gesi unafungwa kwa gharama ya Serikali,” alieleza.



Aidha, alitoa maagizo kwa uongozi wa mkoa kuhakikisha shule hiyo inakamilisha maabara zote nne za sayansi kwa kuzipatia vifaa.



“Wanafunzi wasiendelee kuchora bunsen burner kwenye daftari. Waziione, wazitumie na wajifunze kwa vitendo,” alisisitiza Dkt. Biteko.



Pia alielekeza TANESCO kuhakikisha ndani ya wiki tatu nguzo 25 zinafikishwa kwenye vitongoji ambavyo bado havijaunganishwa na umeme. “Vijiji vyote 52 vina umeme lakini kati ya vitongoji 176, ni 112 tu vyenye umeme. Hali hii inapaswa kubadilika haraka,” alisema.



Dkt. Biteko pia alitoa maelekezo ya kujengwa kwa njia nne za kusambaza umeme kuelekea maeneo ya Loliondo, Namanga, Mundarara na Kamwanga, sambamba na ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme Longido.



Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mundarara, Dkt. Biteko alieleza kuwa madini ni kichocheo kikubwa cha maendeleo, akitolea mfano wa uzalishaji wa madini ya rubi unaoendelea kijijini hapo.


“Nimefurahi kuona Watanzania sasa wana uwezo wa kushiriki katika shughuli za uchimbaji kwa ufanisi,” alisema.



Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini na Mbunge wa Longido, Dkt. Steven Kiruswa, alisema wilaya hiyo imenufaika kwa kiasi kikubwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.



“Wachimbaji wadogo wamepata umeme wa uhakika na katika kipindi cha miaka minne wameingiza zaidi ya shilingi bilioni 9.9,”
alisema.



Dkt. Kiruswa aliongeza kuwa ujenzi wa shule mpya sita za sekondari unaendelea katika kata mbalimbali, huku kata tatu pekee zikiwa hazijafikiwa. Alieleza pia kuwa mgodi wa magadi soda wa Engaruka tayari umetengewa fedha na wawekezaji wapo tayari kuanza kazi.



Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, alisema kuwa maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa TAMISEMI kuhusu ujenzi wa daraja, kituo cha afya na miundombinu mingine tayari yameanza kutekelezwa. 



“Zaidi ya shilingi milioni 250 zimetengwa kwa kituo cha afya na tayari zimeanza kuonekana kwenye mfumo wa fedha. Barabara ya Resingita imetengewa milioni 270, na barabara ya Longido kwenda Meloe imetengewa milioni 105,” alisema.



Dkt. Biteko alihitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa kuchagua viongozi watakaosimamia maendeleo. 



Alisisitiza umuhimu wa kila Mtanzania kutathmini mchango wake katika jamii na kwa taifa.



No comments:

Post a Comment