ASKARI WAPYA WA KJESHI WAHITIMU MAFUNZO KIANGAHAIKO, MKUU WA MAJESHI AWASISITIZA UZALENDO

 


Bagamoyo, Pwani – Aprili 29, 2025

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob John Mkunda, leo ameongoza sherehe za kuhitimisha mafunzo ya awali ya kijeshi kwa Askari wapya katika Shule ya Mafunzo ya Awali ya Kijeshi iliyopo Kihangaiko, Msata, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoani Pwani.





Katika hafla hiyo, Askari wapya walikula kiapo cha utii mbele ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, wakiahidi kuwa waaminifu kwa Taifa na kulitumikia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa moyo wote.





Akizungumza katika sherehe hizo, Jenerali Mkunda aliwataka Askari hao kuzingatia maadili ya kijeshi na kuendelea kuwa na uzalendo wa dhati kwa nchi yao.

“Ninawapongeza kwa hatua hii muhimu ya kuhitimu mafunzo. Nawaagiza mkaende mkatekeleze majukumu yenu kwa kuzingatia kiapo mlichokula. Muwajibike kwa kulinda mipaka ya nchi, kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumtii Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu,” alisema Jenerali Mkunda.

Aidha, aliwasisitiza Askari hao kutunza afya zao ili waweze kuwa na utimamu wa mwili na akili, jambo ambalo ni msingi wa ufanisi katika utumishi wao wa kijeshi.

“Lindeni afya zenu muda wote. Mwanajeshi lazima awe na utimamu wa afya ili aweze kulitumikia Taifa kama alivyosudio,” aliongeza.

Katika nasaha zake kwa Askari wapya, Jenerali Mkunda aliwakumbusha kuhusu misingi minne muhimu ya Mwanajeshi ambayo ni: Nidhamu nzuri, Utii, Uhodari na Uaminifu.

“Zingatieni mambo manne kwa Mwanajeshi – Nidhamu nzuri, Utii, Uhodari na Uaminifu. Taifa linawaamini na kuwategemea katika kuhakikisha usalama na ulinzi wa nchi yetu,” alisisitiza.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kijeshi, ndugu wa wahitimu, na wananchi waliokuja kushuhudia tukio hilo muhimu.

0 Comments:

Post a Comment