Balozi wa Jamhuri ya Korea, Eunju Ahn, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Christian Makonda, ambapo ameahidi kuwa serikali ya Korea Kusini iko tayari kushirikiana na Tanzania katika kubadilishana teknolojia na ujuzi, hasa katika sekta ya uhifadhi wa mazao ya kilimo kama parachichi na mboga za majani kwa ajili ya usafirishaji nje ya nchi.
Akizungumza leo Jumatano, Machi 12, 2025, jijini Arusha, Balozi Ahn amesema, "Tuna nia ya kushirikiana na Tanzania, hususan katika matumizi ya teknolojia ya kisasa ya kuhifadhi mazao ili kuongeza thamani na ushindani wa bidhaa zake katika soko la kimataifa."
Mbali na sekta ya kilimo, Balozi Ahn pia amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa juhudi zake za kukuza utalii na kueleza kuwa Korea itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza mipango ya Rais Samia Suluhu Hassan, hususan kwenye matumizi ya nishati safi kupitia teknolojia ya Bayogesi.
"Teknolojia ya Bayogesi inaweza kusaidia kaya nyingi kutumia nishati safi, huku tukihifadhi mazingira," amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amesema kuwa kutokana na mkoa huo kuwa kitovu cha taasisi za kimataifa na wenye wageni wengi, kuna mpango wa kujenga hospitali kubwa ya kisasa.
"Teknolojia na utaalamu wa Korea katika sekta ya afya unaweza kusaidia kufanikisha azma hii," amesema Makonda.
Ameongeza kuwa mkoa wa Arusha una fursa nyingi za kiuchumi zinazoweza kuvutia wawekezaji wa Korea, hasa katika sekta za usafiri na kilimo.
"Tunawahakikishia wawekezaji mazingira salama ya biashara, utulivu wa kisiasa, na ushirikiano wa dhati kutoka serikalini," ameongeza.
No comments:
Post a Comment