Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje, ambaye pia ni Mgombea wa nafasi ya Umakamu Mwenyekiti wa Bara, amefunguka kuhusu tuhuma zinazomhusu, akisema kuwa alikataa kushirika mapinduzi ya kumwondoa Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe wakati akiwa gerezani.
Ezekia Wenje amedai kuwa sababu kuu ya kutofautiana na Tundu Lissu nna Godbless Lema ni msimamo wake wa kuepuka kushiriki katika mpango wa kumwondoa Mbowe kutoka kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA wakati alipokuwa akishikiliwa gerezani kwa tuhuma za ugaidi.
Wenje amesema kuwa aliona mpango huo kama usaliti na hivyo alijiondoa kwenye msimamo wa kundi hilo.
“Godbless Lema alikuwa kiongozi wa kundi lililotaka kufanya mapinduzi ya kumuondoa Mwenyekiti wa sasa wa chama Freeman Mbowe katika nafasi ili Lissu awe Mwenyekiti,” amesema Wenje.
Aidha, Wenje amesisitiza kuwa aligundua mpango wa Lema na Lissu ambao ulilenga kumtenganisha Mbowe na nafasi ya Mwenyekiti kwa kutumia hali ya Mbowe akiwa gerezani. Alisema, "Ni kweli mimi nilikuwa timu Lissu sasa nimejiondoa kwanini, Mwenyekiti Freeman Mbowe alipokuwa gerezani kwa kesi ya ugaidi, Lema na Lissu walianzisha kampeni ya 'Join the Chain', wakachangisha pesa kwa ajili ya baraza kuu na mkutano mkuu. Walijua Mwenyekiti Mbowe hawezi kutoka gerezani kwa sababu ana kesi ya ugaidi, hivyo ile kampeni yao ililenga Lissu awe Mwenyekiti wa Chadema, nilivyogundua hivyo nikajiondoa, nilikataa usaliti."
Kuhusu pendekezo la Godbless Lema la kumteua Dkt. Wilbroad Slaa katika nafasi ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Wenje amekosoa hatua hiyo, akisema kuwa Dkt. Slaa ameandika vitabu vya kuchafua chama hicho na kwamba ni vigumu kuelewa mantiki ya Lema kumpendekeza kiongozi huyo. "Mtu kama Dkt. Slaa ameandika kitabu on record ya kuchafua chama chetu kila kona ndiyo leo Lema anajaribu kufikiria ateuliwe kuwa Katibu Mkuu. Sijui hiki kitabu akiteuliwa anaenda kukichoma moto au ataenda kuandika kingine cha kureverse haya aliyosema kuhusu chama chetu hiyo pia ni swali lingine," amesema Wenje.
Wenje pia amesisitiza kuwa, yeye anasimama na CHADEMA kama chama na siyo mtu binafsi. "Kuna wengi wameondoka CHADEMA, lakini niwapongeze wanaCHADEMA waliovumilia mateso yote mpaka tumefika hapa, ndiyo maana nasisitiza chama hiki ni kikubwa kuliko mtu yeyote, na mimi nilipojiunga CHADEMA, nilijiunga CHADEMA kwasababu ya itikadi za chama na wala sio itikadi za mtu," amesema Wenje.
Vilevile, Ezekia Wenje amezungumzia kuhusu jinsi alivyohakikisha kampeni zake zinazingatia misingi ya haki, huku akisisitiza kutohusisha vurugu na vitendo vya kutukana wafuasi wa chama kingine. "Sisi katika kampeni yetu hata Mwanza nilisema sitaruhusu mtu yeyote anayeniunga mkono kwenda kumtukana mtu mwingine, kwasababu mwisho wa siku huu uchaguzi utaisha tarehe 21 Januari 2025, kuna siku zingine mbele na maisha yatasonga," amesema Wenje.
Amesema kuwa vitendo vya kutukanana havina tija kwa chama na hata kwa lengo la kisiasa, akiongeza kuwa, "Leo ukimtukana mtu sana halafu mwaka huu tuko kwenye uchaguzi wa Rais wa nchi, anataka kugombea Urais lakini mmeshamtukana sana, nyie mtakwendaje kumsafisha mtu huyo?"

0 Comments:
Post a Comment