Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amewataka wachimbaji wote nchini kuhakikisha wanazingatia sheria na kanuni za sekta ya madini ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima.
Kauli hiyo aliitoa wakati wa kikao kilichofanyika jana jijini Dodoma kilicholenga kutatua mgogoro wa mipaka ya leseni kati ya Kampuni ya Njake na Patrick Miroshi.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Mavunde alizikutanisha pande zote mbili za mgogoro huo na kujadili namna bora ya kutatua tatizo hilo.
Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa wachimbaji wote kuhakikisha wanazingatia sheria katika shughuli zao za kila siku ili kuepuka migogoro ya aina hiyo.
“Serikali inatamani kuona Sekta ya Madini inaendelea kukua na kutoa mchango wa ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Migogoro siku zote inaturudisha nyuma katika jitihada za kuongeza uzalishaji na kuchochea uchumi.
Ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan juu ya utatuzi wa haraka wa migogoro kwenye sekta ya madini ili kuchochea ukuaji wake,” alisema Mavunde.
Aliongeza, “Niwatake maafisa Madini wote nchini kusimamia sheria na kanuni ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima na pia niwatake wachimbaji wote kuzingatia sheria katika shughuli zao za kila siku.”
Baada ya mjadala, timu ya wataalamu iliyoundwa na Waziri Mavunde iliwashauri pande zote mbili kurejea kwenye maeneo ya mipaka ya leseni zao.
Kampuni ya Njake ilielekezwa kumfidia
Patrick Miroshi kwa gharama alizoingia awali za uchimbaji.
Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi wa Wizara ya Madini, akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo.






0 Comments:
Post a Comment