Tuesday, January 14, 2025

Polisi Arusha Waanza Uchunguzi Wizi Ndani ya Gari Toyota Alphard

  

Jeshi la Polisi mkoani Arusha linafanya uchunguzi na kuwatafuta watu wote waliohusika katika tukio la wizi ndani ya gari aina ya Toyota Alphard lenye namba za usajili T. 340 EJR, kama inavyoonekana katika picha zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii.



Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Januari 14, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo, alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 12, 2025, maeneo ya Kaloleni Jijini Arusha. Katika tukio hilo, mtu aitwaye Goodluck Matingisa (41) anadai kuibiwa mali zake.

Kamanda Masejo alisema kuwa uchunguzi bado unaendelea na taarifa zaidi kuhusu tukio hilo zitafikia umma punde. "Bado tunaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hili, na taarifa zaidi zitatolewa," alisema Kamanda Masejo.

Aidha, Kamanda Masejo alitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kubeba vitu vya thamani ndani ya magari yao bila kuwa na ulinzi na kuyaacha maeneo ya maegesho bila ya uangalizi wowote. "Ni muhimu kuwa na tahadhari na mali zenu, hasa mtakapoweka magari kwenye maeneo ya maegesho," alisisitiza.


Sambamba na hilo, Kamanda Masejo aliwaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa kuhusu wahalifu na uhalifu ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na uhalifu. 


"Tunaomba ushirikiano wa wananchi ili kuweza kudhibiti uhalifu na kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake," alisema.

No comments:

Post a Comment