Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani kimesema kuwa baada ya kuhitimisha zoezi la ukaguzi wa magari ya shule (School Bus) kwa kipindi cha likizo, ambacho kilitangazwa ili kuondoa usumbufu kwa wanafunzi wanaotumia vyombo hivyo, kimeanza kuwakamata wale wote walio kaidi agizo hilo huku kikosi hicho kikiwaomba wananchi kuweka uangalizi wa kundi hilo.
Akiongea katika zoezi hilo, Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Zauda Mohamed amesema kuwa kikosi hicho kilitangaza zoezi hilo na kueleza kuwa wameanza operesheni za ukamataji wa magari ambayo hayajakaguliwa na kikosi hicho.
"Kwa sasa tunaanza operesheni ya kuwakamata madereva na wamiliki wa magari ambayo hayajapitia ukaguzi huu, licha ya kuwa tulishatoa taarifa mapema," alisema SSP Zauda Mohamed.
Ameongeza kuwa takwimu zinaonyesha kuna zaidi ya magari 563 ambayo yanatoa huduma kwa wanafunzi, na baada ya ukaguzi huo, imeonekana kuwa bado kuna magari 178 ambayo hayajakaguliwa.
"Kuanzia leo Januari 13, 2025, tunaanza ukamataji wa madereva waliokaidi agizo hili," alisisitiza SSP Zauda.
SSP Zauda pia akatumia fursa hiyo kuwataka wamiliki na madereva wa magari ya shule, kupeleka magari yao katika kikosi cha Usalama Barabarani kwa ukaguzi ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi.
"Watu wote waliokaidi watachukuliwa hatua za kisheria, kwa sababu tunataka kuhakikisha mazingira salama kwa watumiaji hawa," alisisitiza.
Sambamba na hilo, alisema kikosi hicho kinatambua kuwepo kwa kundi jipya la watumiaji wa barabara ambao ni wanafunzi wa shule za awali walioanza shule mwaka huu. Alisema, "Tunawaomba wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuwaelekeza watoto hawa kuhusu matumizi sahihi ya barabara na kuhakikisha wana wasimamizi wakati wa kwenda na kurudi majumbani."
Pia, SSP Zauda alitoa wito kwa madereva kutambua kuwa kuna kundi jipya la watumiaji wa barabara, akiwataka kuchukua tahadhari na kufuata sheria za usalama barabarani ili kundi hilo liendelee kuwa salama kipindi chote. "Ni jukumu letu sote kuhakikisha watoto hawa wanatumia barabara kwa usalama," aliongeza.
No comments:
Post a Comment