Katika tukio la kusikitisha watu watano wa familia moja, wamefariki dunia baada ya kupigwa na radi wakiwa wamelala kwenye kambi ya kuchungia ng’ombe.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia leo, Desemba 29, 2024 likiwahusisha wakazi hao wa Kitongoji cha Nkangi, Kijiji cha Isangawana, Kata ya Matwiga, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, watu hao walifariki dunia baada ya mvua kubwa iliyonyesha usiku ikiwa imeambatana na radi.
“Watu hawa walikuwa wamelala kwenye kambi ya kuchungia ng'ombe wakati walipopigwa na radi, na walifariki dunia papo hapo,” alieleza Kamanda Kuzaga.
Waliopoteza maisha katika tukio hili ni:
- Balaa Scania (39), ambaye ni mfugaji.
- Kulwa Luweja (17).
- Masele Masaganya (16).
- Hema Tati (10).
- Manangu Ngwisu (18).
Aidha, Kamanda Kuzaga alisema kuwa, watu watano wengine walijeruhiwa na walikimbizwa katika Kituo cha Afya Isangawana kwa matibabu.
“Majeruhi hao ni Gulu Scania (30), Manyenge Masaganya (13), Seni Solo (13), Paskali Kalezi (16), na Huzuni Kalezi (19). Walitibiwa na hali zao zilikuwa nzuri, hivyo waliruhusiwa kurejea nyumbani,” alisema Kamanda Kuzaga.
Mwenyeji wa eneo hilo, Mzee Maro, alielezea majonzi makubwa yaliyotawala familia hiyo.
“Ni huzuni kubwa kwetu, familia hii ilikuwa na upendo mkubwa na walikuwa wakifanya kazi kwa bidii. Sisi sote tumeathirika na kupoteza watu hawa wa muhimu,” alisema Mzee Maro.
Tukio hili linatoa wito kwa jamii kuwa makini na mabadiliko ya hali ya hewa, hususani mvua zinazoambatana na radi, ambazo zinaweza kusababisha madhara makubwa kama haya.
Kamanda Kuzaga aliwahimiza wananchi kuchukua tahadhari wakati wa mvua kubwa ili kuepuka madhara ya radi.
0 Comments:
Post a Comment