Desemba 19, 2024, viongozi na wananchi walikusanyika katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam, kuaga mwili wa aliyewahi kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Billy Tendwa, ambaye alifariki Desemba 17, 2024, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika tukio hilo, akitoa salamu za pole na kusisitiza umuhimu wa kuyaenzi mema yote aliyoyafanya marehemu wakati wa uhai wake.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, alimtaja Marehemu Tendwa kama nguzo muhimu katika kujenga demokrasia ya vyama vingi nchini.
Kwa upande wake, Msajili wa sasa wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alisema kifo cha Tendwa ni pigo si kwa familia pekee bali pia kwa wote wanaotambua mchango wake katika siasa ya vyama vingi.
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ally Khatibu, aliongeza kuwa Marehemu Tendwa alikuwa nguzo ya mshikamano wa kisiasa nchini.
Marehemu Tendwa alihudumu kama Msajili wa Vyama vya Siasa kwa miaka 12, kuanzia Mei 2001 hadi Agosti 2013, akiacha historia ya kuimarisha misingi ya demokrasia nchini Tanzania. Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika nyumbani kwao, mkoani Dodoma, ambapo familia, ndugu, na wananchi wataendelea kumuaga kwa heshima kubwa.
Baadhi ya viongozi walioshiki kuaga mwili wa Marehemu Tendwa ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderianaga, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonaz.
No comments:
Post a Comment