Saturday, December 28, 2024

TASAC Yatoa Taarifa Kuhusu Kuzama kwa Meli ya MV. HANIM

 



Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) linatoa taarifa kwa umma kufuatia tukio la kuzama kwa meli ya mizigo ya MV. HANIM, yenye namba za usajili 100326, iliyokuwa imeegeshwa katika fukwe ya Bandari ya Kilwa Masoko (beached) tarehe 27 Disemba 2024. 


Meli hiyo ilisajiliwa Zanzibar tarehe 22 Oktoba 2024. Kwa mujibu wa taarifa ya awali, ajali hiyo haijasababisha kifo wala majeruhi.


Akizungumza kuhusu tukio hilo, TASAC imesema kuwa meli hiyo ilikuwa kwenye safari yake ya kwanza (maiden voyage), ikitokea Bandari ya Mtwara kuelekea Zanzibar. 


Meli hiyo ina uwezo wa kubeba tani 3,500, lakini katika safari hii ilikuwa imebeba mizigo ya saruji tani 3,150. Chanzo cha ajali kilielezwa kuwa ni hitilafu ya kutoboka kwa sehemu ya mwili wa meli (ship hull) upande wa kulia (forward starboard), ambapo maji yaliingia kwenye matenki ya kuhifadhia maji ya mizania (water stability tanks) yaliyopo upande wa kulia. Hali hii ilisababisha meli kutitia upande wa kulia (listing to starboard) na hatimaye kuzama.


"TASAC kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri wa Bahari Zanzibar (ZMA) na mamlaka nyingine za Serikali zinaendelea na zoezi la uchunguzi ili kubaini kama kuna chanzo kingine tofauti na kutoboka kwa meli ili kuchukua hatua za kisheria dhidi ya yoyote aliyesababisha ajali hiyo," inasema taarifa hiyo.


Pia, TASAC imehimiza umma kuzingatia sheria, kanuni, miongozo, na taratibu za uendeshaji wa vyombo vya usafiri majini. Hasa katika ununuzi wa meli zilizotumika, umri wa meli, kufanya ukaguzi wa injini na mwili wa meli (Engine and Ship Bottom Survey), pamoja na kujua mizania na uimara wa meli (Stability and Inclining Test) kabla ya kununua na kusajili meli hizo nchini ili kulinda maisha ya watu na mali zao.


"Tunapenda kutoa rai kwa umma kuzingatia Sheria, Kanuni, Miongozo na Taratibu za Uendeshaji wa Vyombo vya Usafiri Majini hasa katika ununuzi wa meli zilizotumika kuzingatia umri wa meli husika tangu kuundwa kwake, kufanya ukaguzi wa injini na mwili wa meli, pamoja na kujua mizania na uimara wa meli kabla ya kununua na kusajili meli hizo nchini," iliongeza taarifa hiyo.


Kwa wale wanaoshuhudia ukiukwaji wa taratibu za kiusalama au wanahitaji msaada wakati wa dharura, TASAC inatoa wito wa kutoa taarifa kwa Kituo cha Kuratibu Utafutaji na Uokoaji (MRCC) kupitia namba za bure 080011 0101 au 0800110107, au kupitia barua pepe: mrecdar@tasac.go.tz. Huduma hii inapatikana bure masaa 24, siku zote za wiki.


Taarifa hii imetolewa na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC).

No comments:

Post a Comment