Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amemwomboleza Jaji Mwanaisha Kwariko, aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambaye alifariki dunia Desemba 27, 2024 nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.
Katika mazishi ya Jaji Mwanaisha yaliyofanyika Desemba 30, 2024, nyumbani kwa marehemu, Kondoa, Mkoani Dodoma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimwakilisha Rais Dkt. Samia na kutoa salamu za pole kwa familia na waombolezaji.
Akizungumza katika mazishi hayo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kuwa Rais Dkt. Samia ameguswa na kifo cha Jaji Mwanaisha kwani alikuwa ni miongoni mwa majaji wa Mahakama ya Rufani wenye uwezo mkubwa na aliyejulikana kwa weledi na uadilifu katika kazi zake.
“Msiba huu kwetu ni mzito, jukumu letu sisi Wanakondoa, Watanzania, Majaji na wajumbe wa Tume ni kuendelea kumuombea kwa Mwenyezi Mungu,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu alitoa wito kwa wananchi kuenzi mazuri aliyoyafanya Jaji Mwanaisha katika kipindi chake chote cha utumishi wa umma, kwani kufanya hivyo kutakuwa ni njia nzuri ya kuweka kumbukumbu ya kazi zake za kipevu na mfano wa kuigwa kwa vizazi vijavyo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma, alielezea kuwa Jaji Mwanaisha aliishi kwa kiapo cha uadilifu, akiwa mfano wa kiongozi aliyekuwa na ubinadamu na utu.
“Mheshimiwa Mwanaisha alikuwa na ubinadamu na utu, maisha yake yalikuwa ni yakusaidia watu wengine.
Sisi tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwani uhai wake umetusaidia sana katika shughuli mbalimbali za kimahakama,” alisema Jaji Mkuu.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufani) Jacobs Mwambegele, alielezea kuwa Jaji Mwanaisha alifariki dunia wakati Tume ilikuwa inamuhitaji sana, hasa katika mchakato wa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura kuelekea uchaguzi mkuu.
“Tumempoteza Jaji Mwanaisha tukiwa kwenye mzunguko wa nane wa zoezi la kuboresha daftari na tukiwa tunaingia kwenye mzunguko wa tisa utakaohusisha mikoa minne. Aliendelea kutoa ushauri wenye weledi wa hali ya juu,” alisema Mwambegele.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alielezea kwamba Jaji Mwanaisha alikuwa kiongozi mwenye msimamo na mtetezi wa masuala ya wanawake.
“Alibobea katika eneo ambalo alikuwa anafanyia kazi. Sisi Wanadodoma tutamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika masuala ya maendeleo,” alisema Senyamule.
Jaji Mwanaisha Kwariko alifariki dunia akiwa nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.
Kifo chake kimeacha pengo kubwa katika sekta ya haki na maendeleo nchini, ambapo mchango wake utadumu kwa vizazi vingi vijavyo.
0 Comments:
Post a Comment